1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiBenin

Mvutano kati ya Benin na Niger wazidi kutokota

7 Juni 2024

Mwendesha mashtaka nchini Benin amesema mamlaka siku ya Jumatano iliwaweka kizuizini raia watano wa Niger waliodaiwa kuingia kwenye kituo cha bomba la mafuta la Seme-Kpodji nchini Benin huku wakitoa sababu za uwongo.

https://p.dw.com/p/4gl10
Mafuta ghafi
Mkono uliochafuka kwa mafuta ghafi. Mvutano wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi unazidi kutokota kati ya Benin na Niger na hasa baada ya Benin kuwazuia raia wa NigerPicha: AP

Hatua hii inazidisha mzozo kuhusiana na usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Niger kupitia Benin.

Taarifa ya mwendesha mashtaka maalumu Mario Metonou hapo jana imesema kundi hilo liliingia kwenye kituo hicho kinyemela na kuwashtaki angalau wafungwa wawili miongoni mwao wakidaiwa kuwa mawakala wa utawala wa kijeshi wa Niger.

Jana Alhamisi, Waziri wa Mafuta wa Niger Mahamane Moustapha Barke Bako alikana madai hayo na kuwaambia waandishi wa habari kwamba waliokamwa walikuwa ni wakaguzi wa kusimamia upakiaji wa mafuta ghafi kulingana na makubaliano na Benin.

Uhusiano kati ya majirani hao wa Afrika Magharibi umeingia doa tangu Benin ilipozuia usafirishaji wa bidhaa ghafi kutoka Niger kupitia bandari yake mnamo mwezi Mei.