Mzozo wa Saud Arabia na Canada Magazetini
8 Agosti 2018Tunaanzia njia panda inayounganisha Amerika kaskazini na Saud Arabia. Nchi hiyo ya kifalme imekasirishwa mno baada ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Canada kuitolea wito iwaachie huru wanaharakati wa haki za binaadam . Mhariri wa gazeti la "Rheinpfalz" anajiuliza, mbona Marekani imenyamaza? Gazeti linaandika:" Si ajabu kwamba Marekani, jirani wa Canada, haisemi chochote kuhusiana na msimamo mkali wa watawala wa kifalme wa Saud Arabia kuelekea wanaharakati wa haki za binaadam. Mwanamfalme wa Saud Arabia na familia ya Trump akiwemo pia mkwewe Jared Kushner wanasikilizana sana. Kwa hivyo haikuwa sadfa kwa rais Donald Trump kufanya ziara yake ya kwanza nchi za nje katika nchi hiyo ya kifalme ya Saud Arabia. Trump anajisikia vizuri zaidi anapozungukwa na watawala wa kiimla kuliko anapokuwa pamoja na viongozi mfano wa Angela Merkel, Emmanuel Macron na Justin Trudeau."
Masilahi ya kibiashara yanatangulizwa mbele
Gazeti la "Volksstimme" linazungumzia msimamo wa Ujerumani kuelekea Saud Arabia:"Gazeti linazungumzia ishara ya mapambazuko baada ya mwanamfalme Mohammed bin Salman kuruhusu wanawake waendeshe magari katika nchi hiyo inayofuata msimamo mkali wa kihafidhina. Lakini hiyo ni ishara ndogo tu, ikilinganishwa na hasira zilizofuatia lawama za Canada. Wanafunzi 7000 wameamriwa waihame Canada na shirika la ndege la Saud Arabia limesitisha safari zote kuelekea Canada. Pengine jibu hilo la Saud Arabia ndio sababu kwanini serikali kuu ya Ujerumani haijataka kusema lolote kuhusiana na hali namna ilivyo nchini Saud Arabia na hasa kuelekea mvutano pamoja na Canada. Wanaviwanda wa Ujerumani wasingependelea kumuudhi mshirika wao huyo wa kiarabu. Seuze tena kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakifanya biashara nono ikiwa ni pamoja na biashara ya silaha pamoja nao."
Madhara ya vikwazo vya Marekani kwa Iran
Tangu jana awamu ya kwanza ya vikwazo vipya vya Marekani kwa Iran vimeanza kufanya kazi. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linamulika madhara ya uamuzi huo na kuandika: "Kitisho kikubwa zaidi kinahusiana na kuanza upya kufanya kazi mpango wa nuklea wa Iran kwasababu makubaliano yaliyofikiwa kimsingi ndo yameshasitishwa. Umoja wa ulaya usikubali kutumbukizwa chungu kimoja na siasa ya nje ya Marekani isiyoaminika. Gazeti la Mannheimer Morgen linashadidia makubaliano yaliyofikiwa lazima yaheshimiwe."
Matumaini ya sera ya pamoja ya wahamiaji barani Ulaya
Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha katika suala linalozusha mabishano miongoni mwa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya: Wahamiaji. Gazeti la "Fuldaer Zeitung" linazungumzia mkutano kati ya mwenyekiti wa chama cha Christian Democratic Union CDU na mwenzake wa chama cha kisoshialisti cha Uhispania: Gazeti linaandika: "Hata kama misimamo ya viongozi hao hailingani, kimoja lakini ni dhahir mkutano wao utaashiria jambo muhimu: Nalo ni kuibuka mwongozo mpya wa sera ya wahamiaji kati ya nchi za magharibi mwa Ulaya. Sera hiyo haitaziunganisha peke Paris na Berlin, itaenea hadi Madrid. Haimaanishi lakini kama sera hiyo mpya ndio itakayochangia kupatikana ufumbuzi wa suala la wahamiaji barani Ulaya. Mataifa wanachama wanabidi wakubaliane juu ya namna ya kugawana kwa njia za haki mzigo wa wahamiaji pamoja na kuonyesha mshikamano pamoja na yale mataifa yanayoathirika zaidi na wimbi la wahamiaji."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga