1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha Ugiriki kuachana na Euro

19 Machi 2015

Ugiriki inatazamiwa kugubika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels ambako waziri mkuu Alexis Tsipras anapanga kutetea umuhimu wa kupatiwa fedha nchi yake ili kuiepushia balaa la kufilisika.

https://p.dw.com/p/1Et6Q
Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande katika mkutano uliopita wa kilele wa Umoja wa Ulaya mwaka 2014 mjini BrusselsPicha: picture-alliance/epa/O. Hoslet

Ugiriki inatazamiwa kugubika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya baadae hii leo mjini Brussels ambako waziri mkuu Alexis Tsipras anapanga kutetea umuhimu wa kupatiwa fedha nchi yake ili kuiepushia balaa la kufilisika.

Viongozi wa taifa na serikali wa nchi za Umoja wa Ulaya watajadiliana pia kuhusu vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi na huenda wakaamua kuahirisha hadi mwezi wa Juni uamuzi wa kurefusha muda wa vikwazo hivyo kuambatana na jinsi mvutano wa Ukraine unavyoendelea.

Suala la Ugiriki halijaorodheshwa katika ajenda ya mazungumzo lakini ndio suala linalozungumzwa na kila mmoja" duru za Umoja wa Ulaya zinasema.

Mwenyekiti wa baraza la Ulaya,Donald Tusk,ameitisha mkutano kati ya waziri mkuu wa Ugiriki,Alexis Tsipras,,kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliyekataa kuzungumzia kadhia ya Ugiriki katika mkutano uliopita wa kilele,,kati kati ya mwezi uliopita,na rais wa Ufaransa Francois Hollande.Mkutano huo utahudhuriwa pia na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker,mwenzake wa benki kuu ya Ulaya Mario Monti na kiongozi wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro Jeroen Dijsselbloem.

Hofu zimeenea Ugiriki isije ikajitoa katika kanda ya Euro

Majadiliano yao yatahusu mageuzi serikali ya mjini Athens inayotakiwa ipitishe ili iweze kupatiwa fungu jengine-Euro zaidi ya bilioni 7 kutoka jumla ya msaada wa fedha wenye thamani ya Euro bilioni 240 ilizoahidiwa Ugiriki tangu mwaka 2010.

Merkel und Tsipras beim EU-Gipfel in Brüssel am 12. Februar 2015
Kansela Merkel akizungumza na waziri mkuu wa Ugiriki Tsipras,february 12 iliyopita mjini BrusselsPicha: picture alliance/AA

Hofu zimeenea mjini Brussels na katika miji mikuu mengine ya nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu kitisho cha Ugiriki kujitoa katika kanda ya Euro,naiwe kwa khiari au kwa ajali.

Mbali na suala la Ugiriki viongozi 28 wa taifa na serikali za nchi za Umoja wa ulaya wanapanga kuzungumzia pia kuhusu vikwazo ilivyowekewa Urusi mwezi Julai kufuatia kudunguliwa ndege ya shirika la ndege la Malaysia mashariki ya Ukraine.

Mzozo wa Ukraine nao pia utajadiliwa

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya,viongozi wa umoja huo watashadidia kuhusu uwiano uliopo kati ya vikwazo hivyo na kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya amani ya Minsk.

Russland Moskau Feierlichkeiten Jahrestag Krim Annektierung Putin
Rais Vladimir Putin wa Urusi akiadhimisha mwaka mmoja tangu Urusi ilipoimeza raas ya Krimea-mashariki ya UkrainePicha: Reuters/M. Shipenkov

Fikra hapo ni kurefusha vikwazo hadi mwisho wa mwaka ili kuweza kulingana na ratiba ya makubaliano ya Minsk.Lakini viongozi wa taifa na serikali hawatarajiwi kupitisha uamuzi wowote kabla ya mkutano wao ujao wa kilele mwezi juni mwaka huu.

Umoja wa ulaya unapanga pia kubuni "mpango wa kimkakati ili kuivunja nguvu kampeni ya "kupotoa habari kutoka Urusi" kuhusu mzozo wa Ukraine.

Mada nyengine itakayozungumzwa mjini Brussels baadae leo usiku na ambayo inafungamana na mvutano pamoja na Urusi ni kuhusu mradi wa kuundwa Umoja wa nishati miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman