1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nafasi ya kusitisha mapigano Gaza ni finyu

10 Agosti 2014

Majadiliano ambayo si ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza yanatarajiwa kuendelea mjini Cairo leo Jumapili(10.08.2014).

https://p.dw.com/p/1Cs0e
Palästina Israel Luftangriff auf Gaza Stadt 09.08.2014
Mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya GazaPicha: Reuters

Wakati huo huo lakini wajumbe wa majadiliano wa Palestina wameonya kuwa wataondoka mjini humo iwapo ujumbe wa Israel utashindwa kujitokeza.

Shambulio la anga la Israel limesababisha kifo cha Mpalestina mmoja na wengine saba wamejeruhiwa leo(10.08.2014), wamesema madaktari, katika siku ya tatu ya kuanza tena kwa mapigano ambayo yanachafua juhudi za kimataifa za kufikia makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano katika mzozo huo uliodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Palästina Israel Luftangriff auf Gaza Stadt 09.08.2014
Gaza bado inaendelea kushambuliwa na majeshi ya IsraelPicha: picture-alliance/dpa

Pande hizo mbili bado zimeendelea kuwa mbali kimtazamo. Israel inakataa kuwarejesha maafisa wao katika majadiliano ya amani yanayosimamiwa na Misri mjini Cairo kwa kuwa mapigano yanaendelea katika mpaka wa Gaza na Israel. Kiongozi wa ujumbe wa Palestina jana alitishia kujitoa katika mazungumzo hayo iwapo Israel haitabadilisha msimamo wake.

Nafasi ya kusitisha mapigano ni finyu

Msemaji wa kundi la Hamas Sami Abu Zuhri amesema anaona "nafasi finyu sana ya mafanikio ya juhudi za kurejesha usitishaji wa mapigano ambayo yalifikiwa Jumanne iliyopita, na kisha kushuhudia hali ya mvutano ikiongezeka tena kuanzia Ijumaa iliyopita.

London Demonstration zur Unterstützung der Bevölkerung in Gaza 9.8.2014
Maandamano mjini London kupinga mashambulizi ya Israel dhidi ya GazaPicha: REUTERS

Baraza la mawaziri la waziri mkuu Benjamin Netanyahu litajadili mzozo huo katika kikao chake cha kila wiki baadaye leo Jumapili.

"Tuko njia panda na katika muda wa siku mbili ama tatu tutaona iwapo tunaelekea kushoto katika makubaliano , ama kulia katika kuongezeka kwa mzozo huo," waziri wa masuala ya ujasusi Yuval Steinitz, mshirika wa karibu wa Netanyahu, amekiambia kituo cha televisheni cha Channel 10 jana Jumamosi.

Idadi ya vifo inazidi kupanda Gaza

Shambulio la anga la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jebalya mapema alfajiri limesababisha vifo hivyo mjini Gaza , na kuuwa mtu mmoja na kuwajeruhi wengine saba, na kufikisha idadi ya Wapalestina waliouwawa kuwa 1,891 tangu Julai 8 yalipoanza mashambulizi ya Israel ya kuzuwia maroketi kutoka kwa wanamgambo wa Hamas.

Khaled Mashaal bietet Verhandlungen an
Kiongozi wa Hamas Khaled Mashaal mjini CairoPicha: AP

Maafisa wa Gaza wamesema wengi wa Wapalestina waliouwawa ni raia. Israel imesema wanajeshi wake 64 wameuwawa na raia watatu wameuwawa katika mapigano hayo tangu yalipoanza Julai 8.

Israel ilipanua mashambulizi yake ya anga na meli za kivita na kutumia pia jeshi la ardhini kuanzia Julai 17, na iliyaondoa majeshi yake ya ardhini na vifaru kutoka katika eneo hilo siku ya Jumanne baada ya kusema kuwa imeharibu zaidi ya mahandaki 30 yaliyochimbwa na wanamgambo.

Israel imefanya mashambulio ya anga mara 50 dhidi ya ukanda wa Gaza jana Jumamosi(09.08.2014) na kuuwa Wapalestina tisa na wanamgambo wamefyatua maroketi kadhaa dhidi ya Israel wakati mzozo huo ukiingia katika mwezi wa pili, na kuzuwia juhudi za kimataifa kurejesha hatua ya kusitisha mapigano.

UN-Sicherheitskonferenz Israel / Gaza / Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: picture alliance / AA

Ikulu ya Marekani imezitaka Israel na Palestina kufanya kila wanachoweza kufanya kuliwanda raia baada ya kushindwa kurefusha usitishaji mapigano, wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa mapigano zaidi yatazidisha hali ya kibinadamu ambayo hivi sasa ni ya kusikitisha katika ukanda wa Gaza.

Rais Barack Obama na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron wametoa wito wa kumalizika mara moja kwa uhasama.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga