Nagelsmann kocha mpya wa Ujerumani kuelekea Euro 24
22 Septemba 2023Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) lilitangata siku ya Ijumaa kuwa Nagelsmann ndiye atakinoa kikosi cha soka cha Ujerumani kuelekea michuano ya Euro ya mwaka 2024 ambapo Ujerumani ndio itakuwa mwenyeji.
Ujerumani iliachana na Flick mapema mwezi huu, siku moja baada ya kufungwa mabao 4-1 nyumbani na Japan katika mechi ya kirafiki, huku mabingwa hao mara nne wa dunia wakihangaika kupata kuonyesha kandanda safi katika miaka ya hivi karibuni.
Nagelsmann mwenye umri wa miaka 36, kocha wa pili wa timu ya taifa mwenye umri mdogo zaidi katika historia, amesaini mkataba hadi mwisho wa Julai 2024. Wasaidizi wake watakuwa Sandro Wagner na Benjamin Glueck.
Bayern waliachana na Nagelsmann mwezi Machi baada ya kuiongoza kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu. Huko pia alikuwa amechukua mikoba ya Flick akiwa Bayern mwaka wa 2021. Aliiongoza kutwaa taji la ligi ya Bundesliga lakini alishindwa kupata mafanikio ya Champions.
Awali taasisi ya YouGov, iliendesha utafiti kuhusu Julian Naglesmann ambaye alikuwa kocha wa zamani wa mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich.
Utafiti huo umeonesha kuwa ni asilimia 33 tu ya Wajerumani ndio ambao wangependelea Julian Nagelsmann, kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Ujerumani. Wengine 18% wanapinga Nagelsmann kuwa mrithi wa Hansi Flick, wakati 24% hawamfahamu kocha huyo wa zamani wa Bavern Munich.
Ujerumani ilikuwa tayari ina mfululizo wa matokeo mabaya ilishinda mara nne tu katika michezo yake 17 iliyopita.