Namibia na Zambia zatinga robo fainali CHAN
19 Januari 2018Augustine Mulenga , ambaye alifikisha umri wa miaka 28 kabla ya mchezo huo, alifunga bao katika kila kipindi wakati Zambia ikipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cote d'Ivoire katika uwanja wa Grand Stade de Marrakech wenye uwezo wa kuingia mashabiki 45,000.
Baadaye , Namibia ilishinda pambano lake la pili mfululizo kwa bao 1-0 wakati Halleluya Nekundi alipofunga katika dakika za majeruhi dhidi ya Uganda iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani.
Namibia na Zambia zinakutana siku ya Jumatatu mjini Casablanca kuamua nani anashika nafasi ya kwanza na ya pili wakati kutakuwa na pambano la kulinda hadhi wakati Cote d'Ivoire itakapokumbana na Uganda mjini Marrakech.
Ni mara ya tatu katika majaribio matatu ambapo Zambia imefikia awamu ya mtoano katika mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani barani Afrika.
Namibia inashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza baada ya kuishinda Zimbabwe kwa mshangao mkubwa katika michezo ya mchujo, na matayarisho yake yalizuiwa na kufutwa kwa ligi ya ndani ya mwaka 2016/17.
Uganda , ikicheza mchezo wake wa pili chini ya kocha wao mpya Mfaransa Sebastian Desabre , ilimiliki kandanda hadi pale mlinzi wake Timothy Awany alipotolewa nje kwa kadi nyekundi katika dakika za mwisho za mchezo huo.
Namibia ilitumia fursa hiyo dakika mbili katika dakika za nyongeza wakati Nekundi alipofanikiwa kuutumbukiza mpira wavuni mpira ukimpita mlinda mlango Isima Watega kwa shuti la karibu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe