1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Narendra Modi ashinda tena uchaguzi mkuu India

John Juma Mhariri: Josephat Charo
23 Mei 2019

Nusu ya kura milioni 600 zilizopigwa zimeshahesabiwa na data za tume inayosimamia uchaguzi huo zinaonesha kuwa chama cha Modi, kimeshinda viti 300 kati ya viti 543 vya bunge la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3IyJs
Indiens Premierminister Narendra Modi
Picha: Reuters/A. Abidi

Waziri mkuu wa India Narendra Modi mwenye umri wa miaka 68, amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa India na kujipatia muhula mwingine wa kuongoza taifa hilo kwa miaka mingine mitano. Narendra Modi ameahidi kujenga mustakabali utakaowaleta raia wote wa India pamoja.

Chama tawala nchini India cha Waziri Mkuu Narendra Modi Hindu - Nationalist Bharatiya Janata (BJP) kinaelekea kupata ushindi mkubwa kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Nusu ya kura milioni 600 zilizopigwa zikiwa zimeshahesabiwa na data za tume inayosimamia uchaguzi huo zinaonesha kuwa chama cha Modi, kimeshinda viti 300 kati ya viti 543 vya bunge la nchi hiyo.

Aibu kwa Rahul Gandhi

Chama kikuu cha upinzani kimejishindia viti 49 pekee, hali inayomweka mgombea wake Rahul Gandhi katika hatari ya fedheha kubwa ikizingatiwa kwa vizazi vingi, chama hicho kimekuwa na ushawishi mkubwa nchini humo na kiliongozwa na wazee wake Rahul Gandhi waliowahi kuwa mawaziri wakuu na kutokana na ushawishi wao hawakuwahi kushindwa katika uchaguzi nchini humo.

Rahul Gandhi anatoka kwenye famili ya Nehru-Gandhi ambayo imekuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nchini India tangu ilipopata uhuru.
Rahul Gandhi anatoka kwenye famili ya Nehru-Gandhi ambayo imekuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nchini India tangu ilipopata uhuru.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Swarup

Punde baada ya kudhihirika wazi chama cha BJP kinashinda, Narendra Modi aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, kuwa "Kwa pamoja tunakua, tunajiendeleza, tunajenga India yenye nguvu na iliyo imara. India imeshinda tena!” Mwisho wa nukuu. Naye msemaji wa chama BJP Meenakashi Lekhi amesema. "Kwa mara nyingine Narendra Modi atakuwa waziri mkuu wetu. Kazi aliyoifanya kwa miaka mitano na matokeo yake ni bayana mbele ya kila mtu na kila mmoja aliona kazi iliyofanywa kwa kila suala."

Rais wa chama cha BJP Amit Shah naye ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, matokeo ya leo yanaonesha kwamba raia wa India wameondoa utabaka na upendeleo na kuuchagua umoja wa taifa na maendeleo.

Imran Khan ampongeza Modi

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amempongeza Modi kwa ushindi huo unaotarajiwa, na ameahidi kushirikiana naye kuhusu amani na maendeleo ya kanda ya kusini mwa Asia.

Wafuasi wa chama cha BJP washangilia ushindi
Wafuasi wa chama cha BJP washangilia ushindiPicha: DW/O. S. Janoti

Kumekuwa na shangwe katika ofisi za chama cha BJP ikiwemo jijini Mumbai ambapo mamia ya wafuasi na wafanyakazi wamecheza densi huku wakipiga ngoma na nyimbo wakishangilia ushindi.

Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chama cha BJP na washirika wake watapata ushindi mkubwa na watajiongezea viti 50 zaidi.

Hata hivyo hawana wingi wa viti katika baraza la juu la bunge, hali ambayo itakwamisha ajenda za Modi.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, kulikuwa na wapiga kura milioni 900, na uchaguzi ulifanywa kwa duru saba. Matokeo yanatolewa katika awamu tofautofauti hivyo huenda matokeo rasmi yakachukua muda mrefu kabla ya kutangazwa.

Vyanzo: AFPE, DPAE