NATO na EU kushirikiana zaidi kufuatia uvamizi wa Ukraine
9 Januari 2023Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya wanataka kuongeza ushirikiano baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kupindua mfumo wa usalama wa Ulaya.
Haya ni kulingana na azimio la pamoja lililoonekana na shirika la habari la Ufaransa AFP leo. Mashirika hayo mawili yaliyo na makao mjini Brussels, yamekuwa yakitafuta ushirikiano kwa miaka sasa, licha ya hofu kwamba juhudi za kuongeza dhima ya Umoja wa UIaya katika ulinzi huenda zikaiendea kinyume jumuiya ya NATO inayoongozwa na Marekani.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umepelekea wito wa kutumia vyema uwezo wa kiuchumi wa Ulaya na nguvu ya kijeshi ya Marekani, kwa ajili ya kuwalinda watu bilioni moja wanaoishi katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Azimio hilo litatiwa saini na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen.