NATO na Urusi zafanya mazungumzo mjini Brussels
12 Januari 2022Mkutano huo wa leo unafanyika kwenye makao makuu ya Jumuiya ya NATO mjini Brussels baada ya miezi kadhaa yawasiwasi mkubwa barani Ulaya juu ya matendo ya Urusi kuelekea Ukraine.
Na kwa hakika suala kubwa itakuwa ni hizo shaka shaka za mataifa ya magharibi kuwa Urusi huenda inajitayarisha kuivamia kijeshi Ukraine baada ya kuinyakua rasi ya Crimea mnamo mwaka 2014 kutoka nchi hiyo.
Pande hizo mbili zinakutana chini ya mwavuli wa Baraza la Mashauriano kati ya Jumuiya ya NATO na Urusi kwa mkutano wa kwanza tangu mwaka 2019.
Naibu Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Alexander Grushko na mwenzake wa ulinzi Alexander Fomin ndiyo wataongoza ujumbe wa Moscow kwenye mkutano huo.
Marekani yenyewe imemtuma pia naibu waziri wake wa mambo ya nchi za nje Wendy Sherman kuiwakilisha kwenye mkutano unaotarajiwa kuchukua muda wa saa tatu
Matarajio madogo kwenye mazungumzo ya leo
Matarajio ni madogo kwenye mashauriano ya leo lakini Jumuiya ya NATO imesema ina matumaini kuwa mkutano huo utakuwa msingi katika kuendeleza mazungumzo na Urusi siku zinazokuja.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alikaririwa mapema wiki hii akisema mafanikio ya mkutano wa leo itakuwa ni pande hizo mbili kuafikiana kwamba zinaweza kuandaa mikutano mingine siku za usoni.
Katika wakati kiasi wanajeshi 100,000 wa Urusi wakiwa hatua chache tu kutoka mpaka na Ukraine, mkutano wa leo Jumatano utakuwa muhimu lakini bila uwezekano wa kutatua chochote.
Urusi yaweka masharti ya ushirikiano na maelewano
Rais Vladimir Putin wa Urusi amekwishasema masharti ya nchi yake yako wazi, Jumuiya ya NATO ni sharti iaachane na mipango ya kujitanua kwa kuongeza nchi wanachama upande wa Ulaya mashariki.
Putin hapendelei wazo la Ukraine kukaribishwa ndani ya NATO na anashinikiza vilevile Jumuiya hiyo ipunguze shughuli zake kwenye mataifa wanachama yaliyo jirani na Urusi mfano wa Estonia.
Iwapo hayo yatakubaliwa, Moscow iko tayari kuachana na yote yanayotafrisiwa kuwa uchokozi ikiwemo makabiliano ya mara kwa mara ya ndege za kivita kwenye anga za mataifa yanayoegemea upande wa magharibi na manuari za kijeshi kwenye bahari nyeusi.
Mataifa ya magharibi yanapinga masharti ya Urusi
Lakini kile kinachosadifu kuwa kigumu ni kwamba NATO imekwishasema masharti hayo ya Urusi hayakubaliki kwa sababu yatakiuka kipengele muhimu cha mkataba wa kuanzishwa Jumuiya hiyo kinachotoa nafasi kwa taifa lolote kuwa mwanachama iwapo limetimiza vigezo.
Kadhalika mataifa wanachama wa Jumuiya hiyo ikiwemo yale ya Baltiki yaan Estonia, Latvia na Lithuania yanasema mapendekezo hayo ya Urusi ni kichekesho na kwa vyovyote vile hayaingii akilini.
Ukraine yenyewe ambayo itakuwa ajenda kuu ya mkutano wa leo imesema imefarijika na juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na mataifa ya magharibi na ina imani kubwa kuwa NATO haitafikia makubaliano yoyote na Urusi bila kuishirikisha.