Nchi wanachama wa jumuiya ya madola zaijadili Pakistan
12 Novemba 2007Mawaziri hao wa mambo ya nje wa nchi 53 wanachama wa jumuiya ya madola wanadai kurejeshwa mara moja katiba ya Pakistan ikiandamana na uchaguzi ulio huru na wa haki.
Waziri wa mambo ya nje wa Malta Michael Frendo ambae pia ni mwenyekiti wa hatua itakayochukuliwa na kundi la mawaziri hao wa mambo ya nje amesema serikali ya rais Pervez Musharraf lazima izingatie katiba ya nchi.
Kundi hilo la mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 53 wanachama wa jumuiya ya madola wanaweza kusimamisha uanachama wa Pakistana kwa mara nyingine tena kama ilivyotokea mwaka 1999 wakati jenerali Musharraf alipoongoza mapinduzi ya kijeshi.
Uanachama wa Pakistan ulirejeshwa baada ya juhudi nyingi za kidiplomasia kufanyika.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice amesema hatua ya kwanza inayopbidi kufanyika ni kuondoa sheria ya hali ya hatari.
Wakati huo huo kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa zamani nchini Pakistan bibi Benazir Bhutto amesema kuwa amekatiza majadiliano yote na rais Musharraf ishara ya kupinga amri hiyo ya hatari ambayo bado inaendelea.
Bibi Benazir Bhutto kiongozi wa chama cha PPP amewaeleza waandishi wa habari mjini Lahore kwamba amebadili sera zake za hapo awali na hivyo kukatiza kabisa mazungumazo baina yake na rais Pervez Musharraf.
Hatua hiyo ya bibi Bhutto sasa imezua sintofahamu katika muelekeo wake wa kisiasa hasa baada ya kujihusisha katika mazungumzo ya siri na rais Musharraf kwa miezi kadhaa iliyopita yaliyofikia kuondolewa kwake mashtaka ya rushwa yaliyomkabili na hatimae kurudi kwake mwezi uliopita nchini Pakistan kutoka uhamishoni.
Mazungumzo hayo yalihusu chama cha PPP cha bibi Bhutto kumuunga mkono rais Musharraf katika juhudi yake ya kutaka kubakia madarakani kwa muhula wa tatu.
Uhusiano wa viongozi hao wawili uliingia doa tangu Novemba tarehe 3 pale jenerali Musharraf alipotangza hali ya hatari kwa sababu aliyoitaja kuwa ni kupambana na ugaidi hata ingawa wengi wanaamini ilikuwa ni kwa sababu ya kuizuia mahakama kuu kutoa uamuzi juu ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita.
Jamii ya kaimataifa imezidisha shinikizo kwa mshirika huyo wa Marekani kurejesha demokrasia nchini Pakistan.