Nchi za Balkan zataka kujiunga Umoja wa Ulaya
5 Julai 2016Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wamesema uamuzi wa kufadhaisha wa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya hautokuwa na taathira kwa nch za Balkan zinazotaka kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Katika mkutano huo Rais Francoise Hollande wa Ufaransa, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini wamekutana na viongozi wa mataifa ya Balkan na kusisitiza azma yao ya kuendelea na mchakato wa mataifa hayo kuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amewaambia viongozi wa Albania, Bosnia, Kosovo, Macedonia, Montanegro na Serbia ambazo zilikabiliwa na vita katika miaka ya 1990 na ambazo zote zinawania kujiunga na Umoja wa Ulaya kwamba hakuna kilichobadilika kutokana na uamuzi wa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya.
Merkel amesema "Kuna michakato ya kisiasa ambayo bado ni migumu na ndio sababu ni muhimu sana kwa nchi hizi kwamba sote tumesisitiza Rais wa Ufaransa na mimi mwenyewe binafsi na mwanadilomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kwamba mchakato kwa nchi hizo kujiunga na Umoja wa Ulaya inabakia pale pale jambo ambalo nchi hizo zimekuwa zikilihofia.Uamuzi wa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya haukubadili chochote.Cha muhimu ni nchi hizo kutimiza masharti ili kwamba mchakato huo uweze kupiga hatua."
Michakato tafauti
Nchi hizo sita ziko katika hatua tofauti katika michakato yao ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Serbia inakusudia kukamilisha mchakato wake wa mazungumzo ya kujiunga na umoja huo hapo mwaka 2019. Croatia na Slovenia tayari ni nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa nchi za Balkan wamewaambia waandishi wa habari kwamba mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya yanapaswa kuendelea na kwamba hawaogopi kwamba mchakato huo utasitishwa kutokana na uamuzi wa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Albania, Edi Rama, amesema huko Balkan hakuna wanachokiogopa na kuongeza kwamba kura hiyo ya maoni iliopigwa Uingereza itawashawishi viongozi wa Ulaya kwamba mataifa mengi zaidi yanahitajika kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Mchakato kuendelea
Rais Francoise Hollande akizungumza katika mkutano huo wa kilele kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na wale wa mataifa ya Balkan pia amewahakikishia kwamba mchakato wa kujiunga na umoja huo utaendelea:
Ton Hollande amesema "Hapa tuna nchi ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya na tuna nchi ambazo sio wanachama kwa hiyo ni muhimu kusisitiza kwamba uamuzi uliochukuliwa na Uingereza hauweki katika mashaka ahadi zilizotolewa kwa mataifa ya Balkan."
Wakati waliopiga kura kwa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya wanauona umoja huo kuwa unaingilia kati uhuru wa taifa wa kujiamulia mambo yake wananchi wengi wa mataifa ya Balkan kanda iliokumbwa na umaskini na machafuko wanauona umoja huo kuwa nguzo ya utengamano na ustawi.
Kwa upande mwengine nchi za Balkan zinaona kwamba hazipewi kipau mbele na Umoja wa Ulaya hisia ambayo inaweza kupaliliwa na kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.
Mwanishi: Mohamed Dahman /AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef