1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya abiria yaanguka nchini Pakistan

Saleh Mwanamilongo
22 Mei 2020

Ndege ya Shirika la Kimataifa la Ndege la Pakistan (PIA) iliyokuwa na abiria zaidi ya 100 imeanguka leo katika mji wa bandari wa Karachi na kuwaua watu wote 107 waliokuwemo ndani.

https://p.dw.com/p/3cdpj
Wazimamoto wakizima moto kwenye mabaki ya ndege ya kampuni ya kitaifa ya PIA mjini Karachi.
Wazimamoto wakizima moto kwenye mabaki ya ndege ya kampuni ya kitaifa ya PIA mjini Karachi.Picha: Getty Images/AFP/R. Tabassum

Ndege ya Shirika la Kimataifa la Ndege la Pakistan (PIA) iliyokuwa na abiria zaidi ya 100 imeanguka leo katika mji wa bandari wa Karachi na kuwaua watu wote 107 waliokuwemo ndani.

Televisheni ya taifa nchini humo imeonyesha moshi mwingi ukiwa hewani karibu na nyumba ambayo imetoka kujengwa kwenye eneo la tukio. Maafisa wa zima moto walijaribu kuuzima moto kwenye mabaki ya makaazi huku huku helikopta za kivita zikipiga doria juu ya aeneo hilo.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Lahore ilianguka katika eneo la Bustani ya Jinnah mjini Karachi, kusini mwa Pakistan. Hata hivyo, hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu tukio hilo.

''Kulikuwa na abiria 91 na wafanyakazi wa ndege 7 kwenye ndege hiyo iliyopoteza mawasiliano ya anga toka majira ya saa mbili na dakika 37 kwa saa za Pakistan'' alisema Abdullah Hafeez, msemaji wa Shirika la Ndege la Pakistan.

Awali, msemaji wa mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo, Abdul Sattar Khokhar alisema kwamba ndege hiyo ilikuwa na abiria 99 na wafanyakazi wa ndege 8.

Jeshi la Pakistan lilielezea kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba imetuma kikosi cha wanajeshi wa huduma za dharura kwenye eneo la tukio kwa ajili ya msaada wa haraka. Katika miaka ya hivi karibuni, Pakistan imekuwa na rekodi mbaya ya ajali za ndege.