Nelson Mandela - sauti ya uhuru
Neleson Mandela, babu wa Afrika Kusini na shujaa wa mapamabano dhidi ya ubaguzi wa rangi amefariki dunia. Mmoja wa wafungwa maarufu zaidi wa kisiasa wa zama zake, alikuja kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
Kwaheri, Nelson Mandela
Waafrika Kusini wengi watamkumbuka Mandela kwa tabasabu. Walizoea kumuita kwa jina lake la ukoo "Madiba." Kuliko mtu yeyote, Mandela aliunda historia ya taifa jipya la Afrika Kusini. Baada ya kukaa korokoroni kwa karibu miongo mitatu, alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini.
Mwafrika wa kwanza kuasisi kampuni ya uwakili
Nelson Rolihlahla Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 mashariki mwa mkoa wa Cape nchini Afrika Kusini. Baada ya kumaliza shule, aliamua kusomea sheria. Akiwa mwanafunzi alijihusisha zaidi na masuala ya siasa, na mapambano dhidi ya ubaguzi. Mwaka 1952, alifungua kampuni ya kwanza ya uwakili ya waafrika akiwa pamoja na Oliver Tambo mjini Johannesburg.
Ubaguzi wa rangi
Mfumo wa ubaguzi wa rangi, ambao ulikuwa ukiwatenganisha waafrika na wazungu katika kila kitu, uliathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya utoto na hata ujana wa Mandela.
Mandela mwanamasumbwi
Katika umri mdogo, Mandela alikuwa mpenzi mkubwa wa mchezo wa ndondi. "Katika ulingo, hadhi, umri, rangi ya ngozi au utajiri havijalishi," alisema kuhusu mapenzi yake kwa mchezo huo. Aliendelea kujiweka fiti hata alipofungwa: Kama sehemu ya ratiba yake ya kila siku, alibeba vitu vizito na kufanya mazoezi mengine ya kutunisha misuli.
Ahukumiwa kwenda lupango
1964: Jeshi la Polisi likiwarudisha nyuma watu waliokusanyika mbele ya mahakama ambako mashtaka dhidi ya Mandela na wanaharakati wengine wa kupinga ubaguzi wa rangi ilikuwa ikiendeshwa. Katika kesi hiyo iliyopewa jina la Rivonia, Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu ya harakati zake za kisiasa.
Miongo gerezani
Mandela alitumikia miaka 18 katika chumba chenye ukubwa wa mita za mraba tano kilichopo katika gereza la kisiwa cha Roben. Alipewa nambari ya utambulisho 46664. " Nilikuwa nafahamika kama nambari," Mandela alisema baada ya kuachiwa huru.
Mapambano yanaendelea
Wakati Mandela akiwa gerezani, mapambano dhidi ya ubaguzi yaliendelea. Mke wake wakati huo, Winnie Mandela (katikati), alikuja kuwa kiongozi wa mapambano dhidi ya serikali ya weupe wachache.
Dunia yahamasika...
...na hatma ya Afrika Kusini. Tamasha la hisani kwa ajili ya Nelson Mandela lilifanyika katika uwanja wa Wembly mjini London mwaka 1988. Wanamuziki maarufu kimataifa waliadhimisha mwaka wa 70 wa kuzaliwa kwake, na walipaza sauti za kupinga ubaguzi. Karibu watu 70,000 walihudhuria tamasha hilo lililodumu kwa saa 10 na kutangazwa katika mataifa zaidi ya 60.
Hatimaye awa huru
Tarehe 11 Februari, 1990 - baada ya miaka 27 - Mandela aliachiwa kutoka gerezani. Picha hii inamuonyesha pamoja na mke wake Winnie wakiinua mikono juu kuonyesha kujivunia mapambano ya watu weusi dhidi ya utawala wa kibaguzi wa watu weupe.
Arejea katika siasa
Mwezi Mei mwaka 1990, Mandela alirudi katika uongozi wa chama cha Afrika National Congress (ANC) na kuongoza mazungumzo pamoja na rais wa wakati huo Frederik Willem de Klerk (kushoto). Mazungumzo hayo yalisafisha njia kwa Afrika Kusini bila ubaguzi. Mwaka 1993, yeye pamoja na de Klerk walipokea tuzo ya amani ya Nobel.
Washirika wa Mandela
Oliver Tambo (kushoto) na Walter Sisulu (kulia) walikuwa miongoni marafiki wa karibu zaidi wa Mandela. Kwa pamoja waliazisha kikundi cha vijan wa chama cha ANC mwaka 1944, na kuandaa maandamano dhidi ya utawala. Sisulu alihukumiwa maisha jela, Tambo alikaa uhamishoni kwa miaka 30. Baada ya 1990, wote walishika nyadhifa za juu katika ANC.
Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini
Tarehe 10 Mei, 1994 iliingia katika historia. Baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika mwezi Aprili, Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mwafrika. Alitumikia wadhifa huo hadi mwaka 1999, aliporithiwa na Thabo Mbeki.
Maridhiano na si kisasi
Mwaka 1996, Mandela aliunda Tume ya Ukweli na Maridhiano TRC, kusaidia kushughulikia uhalifu uliyotendwa wakati wa utawala wa kibaguzi. Tume hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Afrika Kusini Desmond Tutu. Kazi ya tume hiyo ilikosolewa na wahanga wengi, ambao hawakukubali kwamba wale waliowatendea unyama na kukiri hadharani kutenda unyama huo hawakuadhibiwa.
Maandalizi ya kombe la dunia
Mei 15, 2004 ilitangazwa kuwa Afrika Kusini ndiyo ingekuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la FIFA la dunia mwaka 2010. Hapa Mandela akibeba kombe kwa furaha. Taifa zima liliripuka kwa furaha kutokana na mchango wake alipoisaidia Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa tukio hilo kubwa kabisaa la kimichezo, na la kwanza kufanyika katika bara la Afrika.
Je, taifa la upinde wa mvua limefeli?
Mwaka 2008, chuki dhidi ya wageni na vurugu viliibuka katika maeneo mengi ya madongo poromoka katika miji ya Afrika Kusini, ambamo wahamiaji wengi waliuawa. Swali liliulizwa: Je, hili bado ndiyo taifa la upinde wa mvua lililoasisiwa na Mandela, ambako kila mmoja anaishi kwa amani"? Je, taifa la upinde wa mvua limefeli?.
Miaka ya mwisho ya Mandela
Wakati wa miaka ya mwisho ya maisha yake, Mandela alitoweka katika maisha ya hadhara na kutumia muda mwingi na familia yake. Hapa anaonekana akiadhimisha mwaka wake wa 93 wa kuzaliwa akiwa na wajukuu zake pamoja na vitukuu.