Netanyahu aapa kuendelea na vita Gaza
25 Julai 2024Netanyahu ameyasema haya katika hotuba ya kihistoria aliyoitoa ndani ya bunge la Marekani iliyonuia kutafuta uungwaji mkono katika vita vinavyoendelea katika ukanda wa Gaza.
Kiongozi huyo ameshangiliwa na wanasiasa wengi kutoka chama cha Republican wakati akitoa hotuba yake katika bunge hilo, hotuba hiyo ikiwa yake ya nne ndani ya bunge la Marekani.
Netanyahu ametumia hotuba yake kuwashtumu waandamanaji wanayoiunga mkono Palestina na kuwaita "wajinga wenye manufaa" wanaopokea ufadhili wa siri kutoka kwa Iran.
Hata hivyo, mgawanyiko wa kisiasa kuhusu vita vya Gaza ulijitokeza waziwazi baada ya wabunge kadhaa wa chama cha Democratic kukosa kwa makusudi hotuba ya Netanyahu huku maelfu ya waandamanaji wanaopinga vita vya Gaza wakionekana nje ya bunge.
Rashida Tlaib, mbunge pekee wa Marekani mwenye asili ya Palestina, alibeba bango akimtaja Netanyahu kama "mhalifu wa kivita" na kumshutumu kwa mauaji ya kimbari.