1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu ajadili uwezekano wa kusitisha mageuzi

27 Machi 2023

Viongozi wa serikali ya Israel wamehudhuria mkutano wa dharura ili kujadili jinsi ya kusitishwa kwa mpango wenye utata wa mageuzi ya Mahakama baada ya maandamano makubwa kushuhudiwa jana usiku nchini humo.

https://p.dw.com/p/4PIEB
Israel Protest gegen Justizreform in Jerusalem
Picha: Ilan Rosenberg/REUTERS

Makumi ya maelfu ya watu wenye hasira wanaandamana katika mji mkuu Tel Aviv wakipinga hatua ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu kumfuta kazi Waziri wake wa Ulinzi Yoav Galant baada ya kuitaka serikali kusitisha mageuzi hayo.

Rais wa Israel Isaac Herzog ametoa wito hii leo wa kusitishwa mara moja kwa mpango huo wa mageuzi ya Mahakama ambao waandamanaji wanasema unatishia demokrasia ya Israel.

Netanyahu ameahirisha hotuba yake kuhusu usitishwaji wa mpango huo baada ya Mawaziri kutishia kujiuzulu endapo atafanya hivyo.

Mpango huo ambao ungeliwapa uwezo mkubwa wanasiasa na kupunguza jukumu la Mahakama ya Juu, umetiliwa shaka na washirika wakuu wa Israel ikiwa ni pamoja na Marekani, ambayo ilionyesha wasiwasi wake jana Jumapili.