Netanyahu atishia kuishambulia Rafah
30 Aprili 2024Netanyahau aliyasema hayo siku ya Jumanne (Aprili 30) katika mkutano na jamaa wa mateka na wanajeshi wa Israel ambao walifariki katika vita kwenye Ukanda wa Gaza na kuapa kuendelea na dhamira yake ya mashambulizi dhidi ya Rafah ili kuondosha kile alichodai kuwa ni "ngome zilizosalia za Hamas."
Hata hivyo, washirika wa Israel wameendelea kusisitiza tena na tena upinzani wao dhidi ya oparesheni hiyo, kutokana na wakaazi takribani milioni 2.2 wa Gaza waliokimbia mapigano maeneo mengine kujihifadhi katika mji huo wa kusini.
Soma zaidi: Biden: Sikubaliani na mbinu za Netanyahu huko Gaza
Kauli hiyo ya Netanyahu imekuja wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yakifanyika mjini Cairo, kusaka makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa Israel waliosalia mikononi mwa Hamas na pia Wapalestina wanaoshikiliwa na Israel.