Netanyahu ziarani India
14 Januari 2018Netanyahu na mkewe Sara walilakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini New Delhi na waziri mkuu Narendra Modi ambaye aliandika historia mwezi Julai baada ya kuwa kiongozi wa kwanza wa India kuizuru Israel.
"Ziara hiyo ni fursa ya kuimarisha ushirikiano katika nguvu ya uchumi wa dunia , usalama, teknolojia na uwezo wa kiutalii," Netanyahu alisema katika taarifa kabla ya ziara hiyo.
"Waziri mkuu wa India Modi ni rafiki wa karibu wa Israel na mimi."
Modi ambaye atafuatana pamoja na Netanyahu katika sehemu kubwa ya ziara hiyo ya siku tano , alikumbatiana na waziri mkuu wa Israel mara baada ya kuwasili kabla ya viongozi hao wawili kutoa heshima zao katika eneo la kumbukumbu ya vita katika mji huo mkuu wa India.
"Ziara yako nchini India ni ya kihistoria na maalum. itaimarisha zaidi urafiki wa karibu baina ya mataifa yetu," alisema Modi kupitia ukurasa wa Twitter.
Netanyahu atakuwa ni waziri mkuu wa pili wa Israel kuitembelea India baada ya Ariel Sharon kufanya hivyo mwaka 2003.
Ujumbe wa makampuni ya biashara
Anafuatana na ujumbe mkubwa kabisa wa kibiashara kuwahi kusafiri na kiongozi wa Israel. Viongozi wakuu wa makampuni ya teknolojia , kilimo na ulinzi ni miongoni mwa waliomo katika msafara huo wakati Israel inatafuta makubaliano na taifa hilo lenye uchumi mkubwa wa tatu katika bara la Asia.
Hatua za kuelekea katika ziara ya Netanyahu zilichafuka mwezi huu wakati India ilipositisha makubaliano ya kununua makombora yanayolenga vifaru kutoka kampuni inayomilikiwa na serikali ya Israel ya kandarasi ya masuala ya ulinzi Rafael.
Jeshi la India na serikali vinajadili njia za kufufua maombi ya dola milioni 500, ambayo yalifutwa wakati kampuni ya kandarasi ya masuala ya ulinzi inayomilikiwa na serikali ilipendekeza kutengeneza makombora kama hayo nchini humo.
Israel ni muuzaji mkuu wa sihala nchini India , ikiuza nje wastani wa vifaa vya kijeshi vinavyofikia thamani ya dola bilioni 1 kila mwaka, lakini Modi anataka kufikisha mwisho hali ya India kuwa ni mnunuzi mkubwa wa vifaa vya ulinzi duniani.
Netanyahu na Modi walianza ziara hiyo kwa kutembelea kumbukumbu ya wanajeshi wa India waliopigana katika vita vikuu vya pili vya dunia katika kusaidia kuukomboa mji wa Haifa nchini Israel.
Makubaliano ya kibiashara
Kiongozi huyo wa Israel baadaye atakutana na waziri wa mambo ya kigeni Shushma Swaraj kabla ya kupata chakula cha usiku pamoja na waziri mkuu Modi binafsi.
Netanyahu anatarajiwa kutia saini makubaliano mapya katika nyanja za nishati, usafiri wa anga na utengenezaji wa filamu , pia atatembelea jumba la Taj Mahal, atazuru jimbo anakotoka Modi la Gujarat na kukutana na wacheza sinema maafuru wa Bollywood mjini Mumbai.
Lakini pia atafanya ziara katika kituo cha Wayahudi kilichoshambuliwa mwaka 2008 mjini Mumbai , ikiwa ni ishara ya kuonesha mshikamano na jamii ndogo ya Wayahudi nchini India ambayo inazidi kupungua.
Netanyahu atafuatana na Moshe Holtzberg mwenye umri wa miaka 11 wakati kijana huyo akirejea kwa mara ya kwanza katika nyumba ambako wazazi wake waliuwawa katika mashambulizi hayo ambayo yamesababisha watu 166 kuuwawa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Oummilkheir Hamidou