NEW YORK: Ban Ki-Moon atwaa rasmi wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
1 Januari 2007Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini, Ban Ki-Moon, ametwaa rasmi wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mwanabalozi huyo mwenye umri wa miaka sitini na miwili, alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa nane wa Umoja huo baada ya kuwashinda wagombea sita waliokuwa wakiwania wadhifa huo.
Jana, Ban Ki-Moon alimteua mwanabalozi wa muda mrefu Vijay Nambiar wa India kuwa mkuu wa utumishi wa umoja huo, na mwandishi wa habari maarufu Bi Michele Montas kuwa msemaji wake.
Ban Ki-Moon aliidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa katibu mkuu mwezi Oktoba.
Katibu Mkuu huyo mpya amesema atashughulika ipasavyo kuhakikisha kuwepo amani, maendeleo na ulimwengu wenye haki.
Kipindi cha miaka kumi cha katibu mkuu aliyeondoka, Kofi Annan, kilikamilika rasmi usiku wa kuamkia mwaka mpya.