NEW YORK : Mbeki ashutumu viongozi wa dunia kuzembea umaskini
16 Septemba 2005Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini hapo jana amesema kwamba umaskini ni suala muhimu la usalama na amewashutumu viongozi wa dunia kwa kushughulikia shingo upande kwa woga na kwa kuvuvuwaa hali ya mabilioni ya watu wanaoishi katika mateso ya ufukara.
Akihutubia Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Mataifa katika siku yake ya pili Mbeki ametaja kwamba waraka wa azimio ulioandaliwa kwa ajili ya mkutano huo umekiri kwamba Malengo ya Maendeleo ya Milenia hayawezi kufanikishwa barani Afrika.
Malengo hayo ni pamoja na kupunguza umaskini na njaa angalau kwa watu bilioni moja wanaoishi kwa kutegemea dola moja kwa siku,kuzuwiya kuenea kwa UKIMWI na malaria na kutowa elimu ya msingi yote yawe yamefanikishwa kufikia mwaka 2015.
Mbeki amesema waraka huo ambao mkutano huo wa kilele utauidhinisha leo hii unasema kwa usahihi kwamba muafaka wa usalama unamaanisha kwamba vitisho vya dunia vimefungamana ikiwa ni maendeleo,amani,haki za binaadamu pamoja na ufafanuzi wa asili wa neno usalama.