1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand kuanza kutoa miili ya waliokufa

17 Machi 2019

Mamlaka za New Zealand zinatarajia kuanza kukabidhi miili ya watu waliokufa kwenye shambulizi la misikiti miwili nchini humo, wakati hii leo zitakapoanza kutoa mwili wa kwanza kati ya miili hiyo 50

https://p.dw.com/p/3FCgy
Terroranschlag Neuseeland Trauer Christchurch
Picha: picture-alliance/dpa

Hatua hii itazipa nafasi familia kuanza kuwazika wapendwa wao.

Wachunguzi wa vifo wamesema wanatarajia kutoa angalau mwili mmoja baadae leo Jumapili(17.03.2019) na kuziruhusu familia zinazosubiri kwa hamu kuwazika jamaa zao kwa kuzingatia imani yao ya kidini.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na kusambazwa kwa familia za wahanga hao, watu waliokufa ni wa kati ya umri wa miaka 3-77. Baadhi ya wahanga walitokea maeneo jirani, na wengine walitokea mbali kama vile Misri ama Fiji. Takriban watu wawili miongoni mwa waliokufa- mtoto na baba- walitokea familia moja.

Christchurch Terroranschlag Muslime vor Moschee
Baadhi ya waumini wa Kiislamu wakiwa pembeni ya eneo lililoshambuliwa. Wanalalamikia kucheleweshwa kutolewa miili ya wapendwa wao.Picha: Reuters/J. Silva

Mkuu mmoja wa shule Sheikh Amjad Ali alinukuliwa akilalama, "tayari wameuawa, nini kingine wanataka kujua?", hii ikiwa ni kutokana na kucheleweshwa kutolewa kwa miili hiyo.

Taratibu za dini ya Kiislamu zinaelekeza kwamba mtu akifa anatakiwa kuzikwa katika kipindi cha masaa 24 baada ya kufariki, lakini serikali inataka kujihakikishia kwamba hakuna makosa yoyote yanayojitokeza katika uchunguzi wa miili hiyo, hatua inayochangia kuufanya mchakato wa kuitoa miili hiyo kuwa mgumu.

Mkuu wa wachunguzi hao Deborah Marshall amesema "miili ya waliofariki ilitakiwa pamoaj na mengineyo kufanyiwa vipimo vya mionzi, kuchukuliwa alama za vidole, mpangilio wa meno na kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Arden amesema miili ya waliokufa itaanza kutolewa baadae jioni na kuongeza kuwa wanataraji hadi siku ya Jumatano watakuwa wameikabidhi miili yote kwa familia zao.

Jacinda Ardern
Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Arden ameahidi kubadilisha sheria za umiliki wa silaha.Picha: picture-alliance/AP Photo/New Zealand Prime Minister Office

Akizungumzia shambulizi hilo Arden amesema yeye pamoja na maafisa wenzake 30 walipewa taarifa kupitia barua pepe dakika tisa kabla ya kufanyika shambulizi hilo. Hata hivyo Arden aliongeza taarifa hiyo haikutaja eneo na haikuwa na ufafanuzi zaidi, na ilitumwa pia kwa idara ya ujasusi.

Farid Ahmad mwenye miaka 44 ambaye mkewe Husna aliuawa wakati alipokuwa akikimbilia msikitini kujiokoa, alikataa kumlaumu mshambuliaji na badala yake alisema "ningalipenda kumwambia kwamba nampenda kama alivyo". Alisema hayo alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Kulingana na mamlaka, watu 34 bado wamelazwa hospitalini. Miongoni mwa wanaopambani maisha yao ni mtoto wa miaka wa minne Alin Alsati, aliyekuwa akiswali na baba yake Waseeim katika msikiti wa Al Noor, ambaye alipigwa risasi mara tatu.

Katika hatua nyingine, ahadi ya viongozi wa New Zealand kuimarisha sheria zinazohusiana na umiliki wa silaha nchini humo imekaribishwa na wengi. Waziri mkuu Arden alisema baraza lake la mawaziri litaangazia kwa kina mabadiliko kwenye sheria hiyo kesho Jumatatu. Amesema mapendekezo huenda yakahusisha kuzuia umiliki binafsi wa aina ya bunduki iliyotumika kwenye shambulizi hilo la misikiti.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE

Mhariri: Rashid Chilumba