Ngugi: Kinara wa waandishi Afrika
5 Mei 2014Hakuna anaetunukiwa tuzo ya udaktari wa heshma bila ya kuistahiki. Na Ngugi wa Thiong'o,mwandishi vitabu na mtaalam wa fasihi amefanya mengi yanayostahiki tuzo hiyo.Kitabu chake kilichochapishwa mwaka 1964 kwa kiingereza "Weep Not,Child" au kwa kiswahili "Usilie mtoto" kilikuwa kitabu cha kwanza kuchapishwa kwa Kiingereza na mwandishi vitabu kutoka Afrika Mashariki.
Ngugi wa Thiong'o amesomea katika chuo kikuu maarufu cha Uganda,Makerere, na pia mjini Leeds nchini Uingereza.
Baadae aliamua lakini kuandika vitabu vyake kwa lugha yake ya mama tu,"kikikuyu".Sababu za kutafakari lugha gani itumike ameitaja Ngugi wa Thiong'o katika mahojiano na DW alipoelezea uamuzi wa kuandika mchezo wa kuigiza pamoja na mtunzi mwenzake katika mwaka 1976,Ngugi wa Mirii,na kusema: "Pekee ukweli kwamba tulibidi kujiuliza michezo ya kuigiza tuiandike kwa lugha gani,inatoa picha ya jinsi tulivyogeuka kuwa wageni katika nchi yetu wenyewe kwasababu suala hapo lilikuwa dhahir nalo ni kwamba tuandike lugha inayozungumzwa na walio wengi."
Lugha ya kikikuyu inazungumzwa na zaidi ya watu milioni sita nchini Kenya na ndio lugha ya mama ya Ngugi wa Thiong'o na mtunzi mwenzake Ngugi wa Mirii.
Ngugi wa Thiong'o ameshawahi kufungwa
Kitabu cha mchezo wa kuigiza kilichopewa jina "Ngaahika Ndeenda" au kwa kiswahili "Nitaowa wakati nnaotaka" ingawa kilimpatia umashuhuri mkubwa lakini pia kilimpatia mashaka kutoka serikalini.Kitabu hicho kilipigwa marufuku na mwenyewe Ngugi wa Thiong'o kuwekwa korokoroni kwa muda wa mwaka mmoja.
Lakini kifungo hicho kilimzidishia nguvu za kuendelea kuandika kwa lugha ya kikikuyu.Huko huko jela aliandika kitabu chengine akitumia karatasi za chooni.
Ngugi wa Thiong'o ameshawahi kutunikiwa vyeo kadhaa vya udaktari wa heshima.
Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 40.
Katika hati ya kupatiwa shahada hiyo ya udaktari wa heshima,chuo kikuu cha Bayreuth kinasifu" mchango wake mkubwa unaostahiki kusifiwa wa kueneza fasihi ya kiafrika na hasa fasihi kwa lugha za kiafrika."Vitabu vyake ni msingi wa matumaini ya mageuzi katika uhusiano kati ya Afrika na sehemu nyengine za dunia"-imeandikwa ndani ya hati ya shahada ya udaktari wa heshima ya chuo kikuu cha Bayreuth kwa Ngugi wa Thiong'o.
Mwandishi: Philipp Sandner/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman