Ni miaka 50 tangu kujengwa ukuta wa Berlin
13 Agosti 2011Leo wajerumani wanawakumbuka wahanga wa kuta la Berlin lililojengwa miaka 50 iliyopita. Kwenye hafla iliofanyika katika mji mkuu Berlin, watu walinyamaza kimya kwa muda wa dakika moja ili kuwakumbuka wahanga hao.
Kuta la Berlin lilianza kujengwa siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, na viongozi wa sehemu iliyokuwa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani -yaani Ujerumani ya Mashariki, kwa lengo la kuufunga mpaka kati ya mji wa Berlin ya Mashariki na ya Magharibi.
Ujenzi wa Kuta hilo uliashiria hatua ya kuigawanya Ujerumani wakati huo, hadi tarehe 9 mwezi Novemba mwaka 1989 ambapo kuta hilo liliondolewa.
Jumla ya Watu 136 walikufa katika nyakati mbalimbali walipojaribu kuvuka mpaka kutoka Berlin ya Mashariki ili kukimbilia Berlin ya Magharibi.
Rais wa Ujerumani Christian Wulff atatoa hotuba kwenye hafla hiyo mjini Berlin. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Meya wa jiji la Berlin, Klaus Wowereit, pia wamekuwapo kwenye hafla hiyo.
Mwandishi Maryam Abdalla/dpa/ afp/ epd
Mhariri:Mtullya Abdu