Odinga akataa kuutambua ushindi wa William Ruto
16 Agosti 2022Akizungumza na waandishi habari, kiongozi wa muungano huo, Raila Odinga amesema kuwa hatua hiyo inaliingiza taifa kwenye mkwamo wa kikatiba, kwani mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati amekiuka maoni ya makamishna wenzake alipomtangaza William Ruto kuwa rais mteule.
Kwa mara ya kwanza tangu Tume ya Kusimamia Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, kumtangaza William Ruto kuwa rais Mteule, kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga amevunja kimya chake.
Kwenye mkutano na wanahabari, Raila ambaye sasa amewania kiti cha urais kwa mara ya tano bila ya kufanikiwa amemtaja mwenyekiti wa Tume ya IEBC, Wafula Chebukati kuwa dikteta ambaye aliwaficha makamishna wenzake matokeo hayo kabla ya kuyatangaza.
Soma pia: Ruto atangazwa mshindi wa urais Kenya katikati mwa vurugu
Bila ya kutaja moja kwa moja iwapo ataelekea kwenye Mahakama ya Juu kuyapinga matokeo hayo, Raila amebainisha kuwa watazangatia utaratibu wa sheria kupaza sauti yao.
Raila amedai kuwa matokeo yaliyotangazwa na Chebukati hayakuakisi maamuzi ya Wakenya na ndio maana kulikuwa na mpasuko miongoni mwa makamishna. Makamishna wanne kati ya saba, waliondoka wakati wa kutangazwa matokeo hayo.
Kwa mujibu wa Raila matokeo hayo sasa yanaliingiza taifa kwenye mkwamo wa kikatiba ambao umesabibishwa na IEBC.
Makamishna wanne wa IEBC wajiweka kando na matokeo ya mwisho
Hayo yamejiri huku Naibu wa Mwenyekiti wa Tume ya IEBC Juliana Cherera pamoja na Makamishna watatu wa tume hiyo wakidai kuwa matokeo hayo yalikosa vipengele muhimu vya kumtangaza mshindi. Kwa upande wake Rais Mteule William Ruto amesema kuwa hatalipiza kisasi pindi atakapochukua mikoba ya utawala.
Raila mwenye umri wa miaka 77 ambaye alisusia hafla ya kumtangaza mshindi wa urais, amewataka wafuasi wake kutulia huku wakitafuta njia za kufumbua utata huo.
Soma pia: Kenya: Uchaguzi wa gavana Mombasa na Kakamega waahirishwa
Kwa mara ya Kwanza katika historia ya taifa, Tume ya Kusimamia Uchaguzi, iliyapeperusha matokeo ya uchaguzi huo wa Agosti 9 kwenye wavuti wake na kuhitimisha zoezi hilo, hivyo kuwapa nafasi wadau na vyombo vya habari nafasi ya kujumlisha mahesabu, huku matokeo yakidhihirisha kuwa Ruto alikuwa anaongoza.
Ni hatua ambayo imewafanya waangalizi wa uchaguzi wa taifa na wa Kimataifa, kusema kuwa ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.
Tayari Chebukati ameyachapisha matokeo hayo kwenye jarida rasmi la Serikali, huku kamati ya mpito wa mamlaka ikianza mchakato wa kumkabidhi Ruto ala za urais.
Marais wa mataifa mbalimbali wametuma salamu za pongezi kwa rais mteule, William Samoei Ruto.