Okonjo-Iweala apendekezwa kuongoza WTO
29 Oktoba 2020Siku sita tu kabla ya uchaguzi wa Marekani ambapo biashara ni mada kubwa, serikali ya nchi hiyo imetoa pigo jingine kwa WTO, ambayo Rais wa Marekani Donald Trump anaielezea kuwa "mbaya sana" na ya upendeleo kuelekea China.
Utawala wa Trump tayari umekwamisha jukumu la WTO kuwa mwamuzi wa kimataifa kuhusu masuala ya biashara kwa kuzuia teuzi za jopo lake la rufaa. Sasa unatishia kulifanya shirika hilo kuwa bila kiongozi kwa wiki kadhaa au miezi kadhaa ijayo.
WTO imeitisha mkutano Novemba 9, chini ya wiki moja baada ya uchaguzi wa Marekani, ambapo inatumai itakuwa imepata uungwaji mkono kamili wa kumteuwa Okonjo-Iweala.
Hata hivyo uamuzi huo unahitaji kupitishwa kwa makubaliano, kumaanisha kuwa yeyote kati ya wanachama 164 wa WTO huenda akapinga uteuzi wake.
Baada ya mashauriano, mabalozi watatu wa WTO waliopewa jukumu la kumtafuta mrithi wa Mbrazil Roberto Azevedo, wametangaza jana katika mkutano mjini Geneva kuwa Okonjo-Iweala alipata uungwaji mkono wa kanda zote.
Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara nchini Marekani baadaye ilitoa taarifa ikimuunga mkono rasmi mgombea mwingine pekee aliyebaki, waziri wa biashara wa Korea Kusini Bibi Yoo Myung-hee, ikimsifu kwa kuwa mpatanishi wa mazungumzo yenye mafanikio ya biashara na ujuzi anaohitaji kuongoza shirika hilo la biashara katika "wakati huu mgumu sana."
Pengo la uongozi lilitokea baada ya mkuu anayeondoka wa WTO Azevedo kujiuzulu mwaka mmoja mapema katika mwezi wa Agosti. WTO kwa sasa inaendeshwa na manaibu wanne.
Okonjo-Iweala, waziri wa zamani wa fedha na mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Dunia, atakabiliwa na changamoto kubwa huku madola pinzani yakilumbana wakatzi kukiwa na ongezeko la mivutano na ulinzi wa masoko wakati wa mporomoko wa kibiashara unaosababishwa na janga la virusi vya corona.
Mwandishi: Bruce Amani
Reuters