Olympics 2024: Marekani inaongoza jedwali la medali
7 Agosti 2024Hadi kufikia sasa Marekani imeshika usukani wa jedwali la medali ikiwa imejizolea jumla ya medali 86, 24 za dhahabu, 31 za fedha na 31 za shaba. China imesogea nafasi ya pili ikiwa na jumla ya medali 58 ikifuatiwa na Australia.
Katika soka, Marekani imetinga fainali ya soka la wanawake baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ujerumani katika muda wa ziada na kukaribia kushinda medali ya tano ya dhahabu ya Olimpiki. Marekani sasa itavaana na Brazil katika fainali itakayochezwa Jumamosi.Ufaransa wafungua Olimpiki kwa ushindi, Ukraine waangukia pua
Sweden na Ujerumani zimefikia hatua ya nusu-fainali ya mpira wa wavu wa ufukweni kwa wanaume. Mchezo mwingine ulikuwa ni kikapu upande wa wanaume ambapo Marekani, imeishinda Brazil kwa vikapu 122-87 na kutinga nusu fainali ya mchezo huo.
Na waandaaji wa Michezo ya Olimpiki ya Paris wamesema kwamba mazoezi ya kuogelea katika Mto Seine yamekatishwa kutokana na uchafuzi wa mazingira. Uamuzi huo wa kusitisha mazoezi ambao umetolewa kwa mara ya tano na waandaaji katika mto huo tangu kuanza kwa Michezo ya Olimpiki mnamo Julai 28, unaibua mashaka kwa waogeleaji ambao wanapaswa kufanya mazoezi kabla ya mashindano.