Operesheni za kijeshi Congo zaongezewa muda
2 Juni 2022Uamuzi huo ulichukuliwa katika kikao kilichowaleta pamoja makamanda wa vikosi vya majeshi hayo kilichofanyika jana mjini Fort Port nchini Uganda. Hatua ya kuongeza muda wa ziada kwa operesheni hizo za kijeshi za pamoja inatokea wakati wapiganaji wa kundi la kigaidi kutoka Uganda wa ADF wanazidisha mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Beni, Irumu na Mambasa.
Jana Jumatano, ADF waliwauwa watu wanane katika vijiji vya Beu Manyama na Kabalwa pamoja na kupora nyumba za wakaazi, kikiwemo kituo cha afya.
Akizungumza na wanahabari baada ya kikao hicho, mratibu wa operesheni Shujaa Meja Jenerali Bombele Camille alisema, kuwa awamu ya tatu wa operesheni za pamoja za kijeshi kati ya jeshi la Congo FARDC na lile la Uganda UPDF itawapa fursa ya kuwatokomeza wapiganaji wa kundi la kigaidi ADF, ambao kwa sasa wanashambulia vijiji na wakaazi kwa makundi madogo madogo.
Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha jeshi la Uganda UPDF katika operesheni za pamoja maarufu Shujaa, Meja Jenerali Kayanja Muhanga alisema, kuwa wamepitia operesheni za awali na kwamba duru hii watatizama ni kipi kilichofanywa na kipi kinatakiwa kufanywa kwa sasa ili kupata mafanikio dhidi ya kundi hilo.
"Sijema kwamba ni kipindi muhula mwingine hapana, tumepitia operesheni za awali na kuangalia mafanikio gani tumeyapata tunakotokea na tunakwenda wapi."
Kuongezewa muda wa ziada kwa operesheni Shujaa, kumepokelewa kwa hisia tofauti na wakaazi wa eneo hili, baadhi wakiridhia uamuzi huo ilhali wengine wakipinga. Hawa ni baadhi ya wakaazi tuliokutana nao katika mji mdogo wa Oicha, ukiwa ni mji mkuu wa wilaya ya Beni
Inafaa kuashiria hapa kuwa, operesheni za pamoja kati ya jeshi la Uganda UPDF pamoja na lile la Congo FARDC, zilianzishwa rasmi mnamo Novemba 30 mwaka uliopita, na zilifikia mwisho wake mei 31, pale ADF wakiwa wamepanua zaidi maeneo wanamowashambulia wakaazi.
Baadhi ya mashirika ya kiraia pamoja na yale ya kutetea haki za binaadamu katika maeneo haya, yameelezea nia yao ni kuona majeshi hayo yanaungwa mkono na majeshi ya nchi nyingine wanachama wa jumuia ya nchi za Afrika ya mashariki kwani, kusuasua kwa operesheni dhidi ya ADF, kumesababisha hasara nyingi, kutokana na kuchomwa moto magari, pikipiki pamoja na bidhaa nyingi.
Hadi tunatuma ripoti hii, ripoti kuhusu wanakoelekea wapiganaji wa ADF zimekuwa zikiwakilishwa kwa vyombo vya dola, na inadhaniwa kwamba hatua zitachukuliwa, ili kuwapa raia usalama.
John Kanyunyu DW Beni.