1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza, Ukraine, sera ya ndani vyatia kiwingu urathi wa Biden

20 Desemba 2024

Rais Joe Biden anakabiliwa na changamoto nyingi kabla ya kuondoka madarakani, ikiwa ni pamoja na kusukuma usitishaji mapigano Gaza, kuongeza msaada kwa Ukraine, na kuimarisha sekta ya viwanda nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/4oRVz
Mkutano wa APEC | Joe Biden
Rais Joe Biden anapambana kujenga urathi wake lakini muda hauko upande wake.Picha: Yomiuri Shimbun/picture alliance/AP

Akiwa amesalia na mwezi mmoja tu madarakani, Biden anakabiliana na orodha ndefu ya hatua za sera za ndani na njeanazotaka kukamilisha kabla ya Rais mteule Donald Trump kuingia ofisini, ambapo inatarajiwa kuwa Trump atajaribu kubatilisha mafanikio mengi ya Biden.

Miongoni mwa vipaumbele vya Biden ni kushinikiza usitishaji wa mapigano Gaza, kuachiliwa kwa mateka wa Marekani nje ya nchi, kupeleka msaada zaidi kwa Ukraine, kutoa msamaha kwa wafungwa wasio na hatia ya vurugu, na kusamehe madeni zaidi ya wanafunzi. Aidha, anapanga kutoa ufadhili zaidi kwa uzalishaji wa chipu za semiconductor zinazotumika kwenye vifaa karibu vyote mambeleo vya mawasiliano .

Vilevile, Biden anatazamiwa kuzuia uwezekano wa kuuzwa kwa kampuni ya chuma ya Marekani, kabla ya kuondoka madarakani, hatua zinazolenga kuimarisha urathi wake na kuhakikisha baadhi ya mipango yake inasalia hata baada ya Trump kushika hatamu.

MArekani | Hotuba ya Joe Biden baada ya uchaguzi mkuu wa 2024
Biden aliahidi kurejesha nafasi ya Marekani kama kinara wa dunia katika utawala wake wa miaka minne.Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Orodha hiyo inaonyesha jinsi vita vya muda mrefu na vya umwagaji damu barani Ulaya na Mashariki ya Kati wakati wa uongozi wa Biden vilivyoharibu urathi wake wa kimataifa, ambapo aliahidi kurejesha na kuimarisha uongozi wa Marekani. Wakati huohuo, kushindwa kwa Democrats katika uchaguzi kumeitikisa historia yake ya kisiasa nyumbani.

Soma pia: Biden amkaribisha Trump Ikulu ya White House

Biden, mwenye umri wa miaka 82, aliahidi kubadilisha uchumi wa Marekani akiwa rais na alipata mafanikio makubwa ya kisheria katika nusu ya kwanza ya muhula wake wa miaka minne, ikiwa ni pamoja na miswada ya miundombinu iliyoungwa mkono na vyama vyote, na kupunguza mfumuko wa bei.

Hata hivyo, utungaji mkubwa wa sheria ulisimama kabisa baada ya Warepublican kuchukuwa udhibiti wa Bunge la Wawakilishi katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2022.

Baadhi ya Wademorat wanamlaumu Biden kwa kukataa awali kujiondoa kama mgombea, hatua ambayo wanadai ilisababisha kushindwa kwao vibaya mwezi Novemba, hasa Makamu wa Rais Kamala Harris kushindwa na Trump katika kila jimbo muhimu la uchaguzi.

Trump: Ushindi huu ni mageuzi makubwa ya kisiasa

Vipaumbele vya Biden

Kuhakikisha mpango wa kusitisha vita kati ya Israel na Hamas, ambamo mamlaka ya Wapalestina inasema zaidi ya watu 45,000 wameuawa Gaza, na kuimarisha ulinzi wa Ukraine katika vita vyake vya karibu miaka mitatu na Urusi ni vipaumbele vya juu, kwa mujibu wa maafisa wa Ikulu ya Marekani.

Mwanahistoria wa marais wa Marekani na profesa wa Chuo Kikuu cha Vanderbilt, Thomas Alan Schwartz, anasema si jambo la kawaida kwa marais mwishoni mwa muhula wao au katika kipindi cha mpito kukabiliana na migogoro ambayo haijatatuliwa.

Soma pia: Trump afanya uteuzi mpya, Rubio anatazamiwa kuwa waziri wa mambo ya nje

Mpango wa kusitisha mapigano katika vita vya miezi 14 Gaza unaweza kufikiwa katika siku chache zijazo, huku serikali ikifanya juhudi kubwa za kidiplomasia wiki hii. Majadiliano kama hayo yenye matumaini yamewahi kuvunjika hapo awali, lakini makubaliano haya yana lengo finyu zaidi.

Marekani | Joe Biden akutana na Donald Trump
Joe Biden alipokutana na Donald Trump baada ya uchaguzi, Novemba 13, 2024.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Biden anaharakisha kuisaidia kwa silaha Ukraine kwa hofu kwamba Trump anaweza kukata msaada kabisaa, huku akijaribu kufikia makubaliano ya usalama na Saudi Arabia, licha ya kukataa kwa taifa hilo kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Biden anatarajiwa kuzuia uuzaji wa kampuni ya chuma ya Marekani kwa mnunuzi wa nje wiki ijayo, akitimiza ahadi yake ya kulinda viwanda vya ndani. Kamati ya uwekezaji wa nje ya bunge, CFIUS, ina hadi Desemba 23 kuidhinisha au kukwamisha mpango huo, jambo ambalo hata Trump alisema angefanya.

Soma pia: Je, ni kwa kiasi gani Warepublican wanaweza kubadilisha Marekani?

Hata hivyo, Biden anakimbizana kutekeleza sera nyingine kama kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo Trump anapinga. Wizara za Fedha na Biashara pia zinakamilisha miradi muhimu, ikiwemo uzalishaji wa chip, huku mustakabali wake ukibaki mashakani chini ya Trump.

Chanzo: Reuters