Pakistan yaitaka India kutoa ushahidi
19 Februari 2019Akitoa taarifa yake kupitia runinga ya taifa ya Pakistan, Khan aliitaka India kutoa ushahidi wa kijasusi kuthibitisha madai yake kwamba Pakistan ilihusika na shamulizi hilo lililoua wanajeshi kiasi cha 40 wa India na kuihakikishia kwamba itachukua hatua.
Waziri mkuu huyo alisema wako tayari kufanya mazungumzo kuhusu ugaidi na India ila pia amesema lau India itawashambulia basi wao hawatafikiria mara mbili bali watalipiza moja kwa moja.
Khan alisema kwamba iwapo kuna kundi lolote la waasi linalotumia taifa la Pakistan kufanya mashambulizi basi kundi hilo lina chuki na Pakistan, kwa sababu wanafanya hivyo kinyume na Pakistan.
"Kwa nini Pakistan ifikie hatua hiyo wakati inaelekea katika utulivu? Tumetumia miaka 15 katika vita dhidi ya ugaidi ambapo maisha ya watu elfu sabini yalipotea, wakati utulivu unakuja, wakati ugaidi unapungua, wakati amani imetanda, kwa nini tufanye jambo kama hili? linatununaisha na nini?," alisema Khan.
Juhudi za kimataifa kuingilia kati hali ya India na Pakistan.
Kamishna wa maswala ya haki katika Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet alitoa taarifa akisema anatumai mgogoro huo unaoendelea hautozidi kuvuruga usalama katika mataifa hayo mawili ambayo yote yako na silaha za nuklia,
Kando na hayo Luteni Generali Kanwal Jeet Singh alisema jeshi la India limefanikiwa kuwaua wanamgambo watatu wa kundi la itikadi kali la Jaish-e-Mohammed katika makabiliano ya risasi ambapo wawili waliouliwa ni raia wa Pakistan akiwemo kamanda mkuu wa oparesheni wa kundi hilo huko Kashmir.
Mapema hii leo waziri wa maswala ya kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureishi alimuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kulishughulikia swala hilo kwa udharura akisema linazidi kuwa tishio kwa usalama kufuatia kauli ya India kwamba itatumia nguvu kuikabili Pakistan inayoituhumu kuhusika na shambulizi hilo.
Waziri wa maswala ya kigeni wa Saudi Arabia, Adel Al Jubeir, akizungumza katika mkutano mjini Islamabad, aliahidi kwamba taifa lake litasadia kutuliza hali iliyopo baina ya mataifa hayo mawili ya Asia.
Mwandishi: Faiz Musa/AFP
Mhariri: Hamidou Oummilkheir