Pakistan kufanya uchaguzi wa mapema mkoa wenye watu wengi
16 Januari 2023Hatua hii ni baada ya baada ya kiongozi mkuu wa mkoa huo,ambaye ni mshirika wa waziri mkuu wa zamani Imran Khan kuitisha uchaguzi huo na kusababisha shinikizo kubwa kwa serikali mjini Islamabad. Pakistan inajiandaa kuingia kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu. Kuitishwa uchaguzi wa mapema katika mkoa wa Punjab wenye wakaazi milioni 110 ambayo ni takriban nusu ya idadi jumla ya Wapakistan ni hatua ya gharama kubwa kwa serikali ambayo inategemea msaada wa kigeni na inayojikwamua kutokana na athari za mafuriko. Wachambuzi wanasema kwa kusogezwa karibu uchaguzi wa mkoa huo wa Punjab huenda kukaishinikiza serikali kuu kuitisha uchaguzi wa mapema nchi nzima ili kuepuka gharama ya kufanya uchaguzi mara mbili. Waziri mkuu wa zamani Imran Khan amekuwa akishinikiza uchaguzi wa mapema tangu alipoondolewa madarakani mwezi Aprili mwaka jana kupitia kura ya kutokuwa na imani nae.