Pakistan na India zaadhimisha miaka 60 ya uhuru
14 Agosti 2007Pakistan iliundwa hasa kwa wakaazi wa kiislamu wa kusini-mwa Asia wakati India iliyamua kuwa nchi isioegemea dini wala madhehebu.
Nchi zote mbili zilikwenda vitani maranyingi huku mzizi wa fitina, ukiwa jimbo la Kashmir na kujitenga kwa mashariki ya Pakistan na kugeuka nchi inayofahamika leo Bangladesh.
Kuna mengi yanayo ziunganisha India na Pakistan kuliko yanayo zitenganisha.Na Sura inayotolewa na dola hizi mbili katika vyombo vya habari ulimwenguni, sio sura halisi: Wakati India miaka nenda,miaka rudi ikitoa sura ya nchi ya mafukara,muda mfupi uliopita ikitoa sura ya dola linaloinukia kiuchumi.Pakistan inayotoa sura ya shina la waislamu wenye itikadi kali.
Ukweli wamambo lakini, Pakistan na India licha ya tofauti zao zote na uhasama wao wote,zina mengi ya pamoja: Miongoni mwa hayo, zinastawi kiuchumi,lakini pia taasisi zao za kiraia na kidemokrasia, zinazidi kuimarika.
Vyombo vya habari vya kibinafsi vinatia fora katika nchi zote mbili na hasa TV ambavyo licha ya biashara zinazofanya zimepalilia pia demokrasia nchini Pakistan.
Ushahidi wa hayo ni tokeo la wiki iliopita kuwa si rahisi tu kwa watawala kutangaza hali ya hatari kama watakavyo wao.Rais Musharaf alibidi mpango wake aliouandaa kuurudisha kabatini.Na hivyo fursa ya uchaguzi huru ni nzuri mwishoni mwa mwaka huu.
Hata matatizo yanayozikabili nchi zote mbili-India na Pakistan yanashabihiana:Na hasa matatizo ya kijamii ambayo huko kusini mwa Asia baada ya miaka 60 ya uhuru hayakukaribia hata kupatiwa ufumbuzi wake.Kustáwi kwa uchumi katika nchi zote mbili hakujaufikia umma mkubwa wan chi hizi unaosononeka.
Katika baadhi ya sekta, India imepiga hatua mfano kuondosha hali ya kutojua kusoma na kuandika kwa akina mama au katika mageuzi ya ardhi.Lakini, ile hali ya kuwa sehemu kubwa ya umma licha ya neema ya uchumi wanaishi bado katika ufukara,ni aibu.
India na Pakistan zimekumbwa mnamo miaka michache iliopita na balaa la m achafuko ya kidini na mchanganyiko wa dini na siasa.Wakati nchini India chama cha wahindi kinaendesha serikali ,huko Gujirat waislamu walio-jamii ya wachache wakiandamwa na kutimuliwa makwao.
Nchini Pakistan chuki zinapaliliwa na umma dhidi ya kambi ya magharibi; na wanajeshi na idara za usalama zina mafungamano makubwa na waumini wenye itikadi kali ya kiislamu.
Kwahivyo,kuadhimisha siku ya leo na kesho ya uhuru wa Pakistan na India, licha ya mengi yanayoziunganisha nchi hizi mbili,haitoshi kusherehekea pamoja.Vikundi vya kiraia vilivyopanga katika maeneo ya mpakani kufanya tafrija na burdani za pamoj, vilizuwiliwa. Labda pale India na Pakistan zitakapo adhimisha miaka 70 ya uhuru ,itawezekana kusherehekea pamoja.