Pakistan yapeleka jeshi mpakani na India na kufuta likizo za wanajeshi
26 Desemba 2008Uhusiano kati ya nchi hiyo jirani za Asia ya Kusini umeathirika sana tokea mashambulizi dhidi ya mji wa Mumbai nchi India kuuwa watu 179 ambayo serikali ya India inawalaumu wanamgambo walioko Pakistan kwa kuhusika nayo wakati serikali ya Pakistan ikisema kwamba India haikuipa ushahidi wa kuifanya nchi hiyo ichukuwe hatua.
Msemaji mkuu wa majeshi ya Pakistan Meja Generali Athar Abbas amekataa kuzungumzia hatua hiyo ya Pakistan lakini afisa mwandamizi wa wizara ya ulinzi amethibitisha kwamba baadhi ya vikosi vimekuwa vikihamishwa kutoka eneo tete la kaskazini magharibi karibu na mpaka na Afghanistan na kupelekwa kwenye mpaka na India.Amesema likizo za wanajeshi wote wa ulinzi zimefutwa kama hatua ya kujihami.
Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh amekutana na wakuu wa vikosi vya ardhini, wanamaji na anga kujadili malipo ya kijeshi ambapo pia amezungumzia hali ya mvutano kati ya nchi hiyo na Pakistan.
Wachambuzi wengi wa mambo wanasema ni jambo lisiloyumkinika kwamba mvutano huo utazitumbukiza nchi hizo vitani.
Nchi hizo zenye kumiliki silaha za nuklea zimepigana vita vitatu tokea uhuru hapo mwaka 1947 na zilikuwa kwenye ukingo wa vita vya nne hapo mwaka 2002 kufuatia shambulio dhidi ya bunge la India.