Pakistan yataka kushirikiana na India kuangamiza ugaidi
15 Julai 2010Mkutano wa mjini Islamabad umelenga kuyafufua mazungumzo ya amani yaliyovunjika na kurejesha uhusiano wa kawaida baada ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuingia doa kufuatia mashambulio ya kigaidi ya mwaka 2008 katika mji wa Mumbai.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Pakistan, Shah Mehmood Qureshi na mwenzake wa India, S M Krishna wameanza rasmi mazungumzo yao kwa kipindi maalum cha upigaji picha katika wizara ya kigeni ya Pakistan mjini Islamabad hii leo. Afisa wa wizara hiyo amesema mkutano kati ya mawaziri hao umefanyika katika mazingira ya kirafiki na kwamba yapo matumaini ya kupiga hatua mbele katika juhudi za kuufufua mchakato wa kutafuta amani kati ya India na Pakistan.
Mkutano huo ni wa kwanza wa aina yake kuwahi kufanyika kutafuta maridhiano na kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya India na Pakistan tangu mashambulio ya kigaidi dhidi ya mji wa Mumbai mnamo mwaka 2008. Mazungumzo kati ya India na Pakistan yamekuwa yakikabiliwa na vikwazo tangu miaka mingi kwa sababu pande zote mbili zina mawazo tofauti kuhusu masuala yanayotakiwa kujadiliwa. Huku Pakistan ikiuona mzozo wa jimbo la Kashmir kuwa ufunguo wa uhasama kati yake na India, India kwa upande wake inataka kujadili jukumu la Pakistan katika kudhamini mashambulio ya kigaidi na harakati za makundi ya wanamgambo nchini India.
Mtaalam wa uhusiano kati ya India na Pakistan, mjini New Delhi, Suba Chandran, anasema, "Mazungumzo jumla ni mapana. Makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1998 yanatoa msingi mzuri wa mazungumzo yoyote katika siku za usoni. Nitafurahi kama nchi zote mbili zitayazingatia makubaliano hayo kwa kuwa yanatoa muelekeo kuzungumzia masuala yote kuhusu nyuklia na biashara."
Waziri wa mambo ya kigeni wa India, SM Krishna amekutana pia na waziri mkuu wa Pakistan, Yousuf Raza Gilani na rais Asif Ali Zardari katika neo lililo chini ya ulinzi mkali la "Red Zone" ambako ni makao ya afisi za serikali na balozi za nchi za kigeni katikati ya mji mkuu, Islamabad.
India inalilaumu kundi la Lashkar-e-Taiba (LeT) la nchini Pakistan kwa mashambulio yaliyofanywa na wanaume 10 waliowaua watu zaidi ya 160 na kusitisha mchakato wa miaka mitano wa kutafuta amani kati ya nchi hizo mbili za Asia Kusini ambazo zimepigana vita mara tatu tangu zilipojipatia uhuru wao kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1947.
Pakistan imekiri kwamba mashambulio ya Mumbai kwa sehemu fulani yalipangwa katika ardhi yake na kuwatia mbaroni washukiwa wasiopungua saba, akiwemo kiongozi aliyeyaongoza mashambuo hayo, Zakiur Rehman Lakhvi. India inaitaka Pakistan iwajumulishe washukiwa zaidi kwenye uchunguzi wake, akiwemo Hafiz Saeed, anayedhaniwa kuwa muasisi wa kundi la LeT, ambaye alikamatwa na baadaye kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi wa kutosha.
Suba Chandran, mtaalam wa uhusiano kati ya India na Pakistan, mjini New Delhi, anasema mazungumzo ya leo mjini Islamabad hayatafua dafu katika kuyafufua mazungumzo ya amani kwa kuwa Pakistan inasita kushirikiana.
"Hakuna uwezekano wa Pakistan kuwawasilisha washukiwa hao kwa kuwa ni suala la kisiasa. India imeeleza wazi msimamo wake na inaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa. Hakuna kinachoweza kufanyika. India inatakiwa kuzungumza na jirani yake."
Mazungumzo ya leo yamegusia pia mzozo wa jimbo la Kashmir, ambalo India na Pakistan zinadai ni himaya yake. Mkutano umegubikwa na madai ya waziri wa mambo ya ndani wa India, GK Pillai kwamba shirika la ujasusi la Pakistan lilihusika katika shambulio la mjini Mumbai, kwa kusimamia na kuratibu mipango yote tangia mwanzo hadi mwisho. Pillai amenukuliwa akisema ushahidi ulijitokeza wakati alopihojiwa mshukiwa wa ugaidi, David Headley, raia wa Marekani ambaye anazuiliwa na maafisa wa Marekani.
Mwandishi: Josephat CharoBärthlein, Thomas (DW Südasien)/ZPR
Mhariri: Abdulrahman