Pambana! Waafrika Mashariki wakabiliana na ukoloni
21 Desemba 2023Kwa nini Ujerumani iliidai ardhi ya Afrika Mashariki?
Awali, kuwepo kwa Wajerumani katika Afrika Mashariki kulikuwa kumejikita tu kwenye uporaji wa ardhi uliofanywa na wakoloni binafsi kama vile Carl Peters. Kwenye Mkutano wa Berlin mwaka 1885, Ujerumani ikadai ardhi ya Tanzania Bara, Rwanda, na Burundi za leo, ambazo ziliwapa mamlaka ya kuanzisha, kudhibiti na kulinda njia ya biashara.
Vipi ukoloni wa Ujerumani ulikuwa wa kikatili?
Mwaka 1888, makaazi ya walowezi wa Kijerumani katika Mwambao wa Afrika Mashariki yalishambuliwa wakati wa Vuguvugu la Abushiri, ama la Vuguvugu Waarabu. Vuguvugu hilo lilikuwa ni mchanganyiko wa wapiganaji wa Waswahili wa Mwambao wenye mafungamano na kiongozi wa wenyeji, Abushiri bin Salim al Harth, ambao walikuwa hawataki Ujerumani idhibiti njia zao za misafara ya biashara ya pembe za ndovu na watumwa. Kijuujuu, Ujerumani ilihalalisha matumizi ya silaha na wanajeshi kama njia ya kukomesha biashara ya utumwa, lakini kiuhalisia, silaha na wanajeshi hao walitumika kulinda maslahi ya Ujerumani.
Je, Ujerumani ilikuwa na jeshi?
Awali, kikosi cha kikatili cha Wissmann, ambacho ndicho chimbuko la kile kiitwacho kwa Kijerumani "Schutztruppe" (Kikosi cha Ulinzi), kilichokuwa kikiongozwa na Hermann von Wissmann, kiliivamia Afrika ya Mashariki kikiwa na silaha za kisasa kama vile bunduki za Maxim Machine. Walikuwa na kiwango cha chini cha uwajibikaji na hawakuwa wanamgambo rasmi wa Ujerumani, kwani askari wake wengi walikuwa makuruta wa Kiafrika. Watu hawa, wakiongozwa na maafisa wachache wa Kijerumani, walikuwa na nafasi kubwa ukatili uliokuwa ndiyo taswira hasa ya utawala wa Ujerumani katika Afrika Mashariki. Unyogaji, ubakaji na wizi ukafuatia, na kufikia mwaka 1890, mwambao wote wa Afrika ya Mashariki ukawa tayari chini ya udhibiti wa Ujerumani.
Kisha wakoloni hao wakaelekeza macho yao ndani ya bara kuelekea Ziwa Tanganyika, ambako walikabiliana na upinzani mkali. Katika jumla ya makabiliano hayo na wenyeji, yumkini hakukuwa na yaliyokuwa maarufu zaidi kama yale yaliyoongozwa na kiongozi wa Wahehe, Chifu Mkwawa.
Nani alikuwa Chifu Mkwawa?
Alikuwa kiongozi wa kabila la Wahehe wenye makao yao mkoani Iringa katika Tanzania ya sasa. Mkwawa alikuwa mwanadiplomasia wa kiwango cha juu na mwanamikakati mkubwa wa kijeshi kama alivyodhihirisha kwenye makabiliano yake na kamanda wa kikoloni wa Kijerumani, Emil Zelewski, ambaye baadhi ya wanahistoria wanajenga hoja kwamba ndiye aliyechochea Uasi wa Waarabu wa mwaka 1888. Zelewski alipewa jukumu la kuwaangamiza Wahehe, na alitumia mbinu za nyingi za kikatili kama vile kuangamiza ardhi, kuchoma mashamba, kuuawa na kuharibu mifugo.
Wakiwa wamejihami kwa mishale na bunduki chache, Wahehe waliwazunguka na kuwauwa wanajeshi wengi wa Zelewski, akiwemo Zelewski mwenyewe, mwaka 1891. Kushindwa huku lilikuwa jambo la aibu kubwa mno ambalo wakoloni wa Kijerumani hawakuja kulisahau. Na ingawa Wahehe walipigana vita vya msituni, hatimaye Mkwawa alizungukwa kabla hajaamuwa kujiuwa mwenyewe mkoani Iringa mwaka 1898. Mkwawa alichukiwa mno na wakoloni wa Kijerumani kiasi cha kwamba baada ya kufa, kichwa chake kilichukuliwa na kupelekwa Berlin.
Kipi kilimtokea Mangi Meli?
Mangi Meli, mtawala wa Mlima Kilimanjaro, ambaye naye pia alivamiwa na kulazimishwa kujisalimisha. Yeye pamoja na viongozi wengine wa jamii ya Chagga walinyongwa mwaka 1900 kwa tuhuma ya uhaini. Mauaji hayo sio tu yaliharibu mfumo wa uongozi wa wenyeji, bali pia yalikithiri ubaya wake pale mamlaka za ukoloni wa Kijerumani zilipomkata kichwa Mangi Meli na vufu lake kupelekwa Berlin kwa utafiti wa kibaguzi wa anthropolojia na sayansi. Hadi leo, fuvu la Mangi Meli limehifadhiwa kwenye makumbusho moja nchini Ujerumani.
Viti vya Maji Maji vilikuwa nini?
Mnamo mwaka 1905, zaidi ya makabila 20 yaliunganika chini ya Kinjeketile Ngwale na kupambana na utawala katili wa Kijerumani, ambao uliwalazimisha kulipa kodi na kuwafanyisha kazi kwa nguvu. Kwa namna fulani, Kinjeketile mwenyewe alikuwa mtu mwenye utata, kwa sababu alisambaza utabiri kwamba wapiganaji wenyeji wangeliweza kuwafurusha wavamizi wa Kijerumani na walipaswa kutumia mtama na maji kuzigeuza risasi za wakoloni kuwa maji. Hiki kilihamasisha ule uliokuja kufahamika kama uasi wa Maji Maji, japokuwa baadhi ya wanahistoria wanaamini kuwa utabiri wa Kinjeketile ulikuja katika wakati ambapo wenyeji hawakuwa na namna nyengine yoyote isipokuwa kuuasi utawala wa Kijerumani.
Ingawa makabiliano ya mwanzo yalifanikiwa kuuwa baadhi wa wamishionari na walowezi wa Kijerumani, lakini muda mfupi baadaye uasi huo wa Maji Maji ulishindwa na kuwageukia wenyeji, ambapo mamlaka za kikoloni ziliendesha kampeni kali ya adhabu. Kinjeketile pia aliuawa mwaka 1905.
Hata baada ya Kinjeketile kuuawa, jeshi la "Schutztruppe" liliendeleza mbinu zake za kuangamiza ardhi, mauaji na ugaidi kwenye eneo zima la Afrika Mashariki. Na ilikuwa imepangwa hivyo kimkakati.
Uasi wa wenyeji uliendelea hadi mwaka 1907, ukiwa umegharimu maisha ya zaidi ya watu 120,000, na wengine wanakisia kuwa idadi ilifikia hadi 300,000, ambapo watu wengi walikufa kwa njaa na maradhi.
Mfululizo huu wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.