1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pope ahimiza huruma kwa wanawake na watoto wanaonyanyasika

21 Novemba 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amehimiza juhudi zaidi katika kupambana na fedheha zinazowakumba wanawake na watoto wanaolazimishwa kujiingiza kwenye biashara ya ngono.

https://p.dw.com/p/3TTfl
Thailand Bangkok.  Besuch Pabst Franziskus
Picha: picture-alliance/Zuma/C. Subprasom

Amesema hayo wakati anapoanza ziara yake nchini Thailand hii leo ambako umasikini na biashara haramu ya binaadamu kwa pamoja vimechangia kuchochea biashara hiyo ya ngono. 

Wakati akifungua misa takatifu ya wazi iliyofanyika kwenye uwanja wa taifa wa michezo ulioko mjini Bangkok Papa Francis amelaani adhabu zinazowaumiza masikini kwenye eneo hilo. Amewahimiza Wathai kutopuuzia wanawake na watoto wanaosafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono ama wahamiaji wanaofanya uvuvi na ombaomba.

20.11.2019 Matangazo ya Asubuhi

Ameliambia kusanyiko la waumini karibu 60,000 waliokuwepo uwanjani hapo kwa ibada ya jioni kwamba "wote hao ni sehemu ya familia zetu, ni mama zetu, kaka na dada zetu".

Thailand Besuch Pabst Franziskus Messe Stadion
Wakatoliki kutoka makabila ya Thailand wakimsubiri Papa kuanza ibada kwenye uwanja wa michezo, BangkokPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Lalit

Umoja wa Mataifa unaitaja Thailand kama kitovu cha biashara haramu ya binaadamu pamoja na chanzo cha kazi za kulazimishwa na ngono wanaosafirishwa ndani ya mipaka ama nje ya nchi hiyo. Ripoti ya mwaka huu ya taasisi ya Umoja huo inayoshughulikia dawa za kulevya na uhalifu imesema biashara haramu ya binaadamu kwa ajili ya biashara ya ngono imechangia asilimia 79 ya visa vyote vya usafirishaji wa binaadamu nchini Thailand tangu mwaka 2014 hadi 2017.

Miongoni mwa wahanga 1,248 waliotambuliwa, asilimia 70 walikuwa ni wasichana wadogo.

Waumini takriban 60,000 wamehudhuria ibada hiyo huku wengi wakionyesha shauku kubwa ya kumuona kiongozi wao wa kidini. Ryan Arquiza ni miongoni mwao.

"Nimetokea Ufilipino na nimekuja hapa Thailand kumuona Papa. Nimekulia familia ya Kikatoliki, kwa hiyo ni kitu kikubwa sana kumuona papa kwa macho yangu. Nahisi kubarikiwa sana kuungana na Wakatoliki wa Thailand, kusherehekea pamoja na mimi mwenyewe kumuona Papa." amesema muumini huyo wa Kikatoliki.  

Mapema Papa Francis alieleza kuridhishwa kwake na juhudi za serikali za kupambana na janga la biashara haramu ya binaadamu katika hotuba yake ya kwanza aliyoitoa alipokutana na waziri mkuu wa Thailand Prayuth Cha-o-cha, kwenye mkutano mfupi wa faragha ofisini kwake

Thailand Papst Franziskus in Bangkok
Papa Francis akiwa kwenye hekalu ya Wat Ratchabophit alipokutana na kiongozi wa juu wa Buddha.Picha: Getty Images/AFP/V. Pinto

Hata hivyo, alitoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuwajibika kuwalinda wanawake na watoto ambao haki zao zinakiukwa kwa kuingizwa kwenye kila aina ya unyanyasaji kama utumwa, mateso na dhuluma akitoa mwito wa kutafutwa njia za kuondoa uovu na kurejesha utu wao.

Kwenye hotuba yake kwa Papa waziri mkuu Prayuth amesisitizia kwamba Thailand imepiga hatua kubwa katika kuhamasisha haki za binaadamu na kuendeleza mahusiano na taasisi za kimataifa.

Papa Francis pia amekutana na kiongozi wa juu wa waumini wa Buddha kwenye hekalu la Wat Rachabophit ambako alitoa mwito kwa Wakatoliki kushirikiana na waumini wa Buddha ambao ni wengi zaidi nchini Thailand kuanzisha miradi ya kuwajali masikini na mazingira.

Kesho Ijumaa atakuwa na mkutano na viongozi wa imani mbalimbali nchini humo kabla ya kuondoka kwenda Japan.