Papa ataka usawa kwa wahamiaji
8 Julai 2013Akizungumza leo wakati wa Ibada ya Misa Takatifu katika kisiwa cha Lampedusa, Baba Mtakatifu Francis amewaomba radhi wahamiaji na wakimbizi kutokana na vitendo visivyo vya kibinaadamu ambavyo wamekuwa wakifanyiwa na kutoa wito wa dunia kuangalia upya dhamira zao ili kumaliza tofauti hizo.
Ibada hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa michezo ambao hutumika kama kituo cha kuwapokea maelfu ya wahamiaji kutoka Afrika Kaskazini, imehudhuriwa na wahamiaji 166 waliowasili Lampedusa na kuungana na maelfu wengine ambao wameingia kwenye kisiwa hicho wakitokea Afrika ya Kaskazini tangu kuanza kwa vuguvugu la mapinduzi katika nchi za Kiarabu mwaka 2011.
Atupa shada la maua kwenye maji
Kabla ya kuanza kwa Ibada hiyo ya Misa, Baba Mtakatifu Francis, ambaye yeye mwenyewe ni mtoto wa wazazi wahamiaji kutoka Italia walioingia Argentina, aliweka shada la maua katika kisiwa cha Lampedusa, ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka maelfu ya wahamiaji kutoka Afrika ambao walikufa wakati wakijaribu kuingia barani Ulaya kwa kutumia usafiri wa majini usio salama.
Akiwa ndani ya boti, Baba Mtakatifu alirusha shada hilo la maua kwenye maji baada ya kuwasili kwenye kisiwa hicho, hiyo ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya mji wa Roma tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki duniani mwezi Machi, mwaka huu.
Baada ya kuwasili kisiwani humo, Baba Mtakatifu alizungumza na wahamiaji vijana kutoka barani Afrika na baadae anatarajiwa kutakutana na wakaazi wa kisiwa hicho kutoka jamii ya wavuvi.
Ziara hiyo kuonyesha mshikamano
Mkurugenzi wa Baraza la Kiitaliano kwa ajili ya wakimbizi, Christopher Hein, ameliambia gazeti moja la Kikatoliki kuwa ziara hiyo ya Baba Mtakatifu Francis ni ishara muhimu ya kulizingatia suala la wahamiaji, huku kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani akiwa na matumaini kwamba ziara yake hiyo itatoa hamasisho kuhusiana na tatizo hilo.
Kwa upande wake, Mwadhama Antonio Kardinali Mario Veglio, mkuu wa idara ya wahamiaji ya Vatican, amesema ziara hiyo itaonyesha mshikamano na kuimarisha hali ya wahamiaji ambayo kwa sasa wamekuwa wakifanyiwa vitendo ambavyo havikubaliki.
Aidha, Meya wa kisiwa cha Lampedusa, Giusi Nicolini ameomba msaada zaidi katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la wahamiaji wanaoingia kisiwani hapo pamoja na ndani ya Italia yenyewe na barani Ulaya kwa ujumla. Tangu mwaka 1999, zaidi ya wahamiaji 200,000 wameingia Lampedusa, wakiwa na nia ya kuvuka mpaka wa Ugiriki na Uturuki, moja ya njia kuu kwa wahamiaji wasio na vibali maalum pamoja na wakimbizi wanaotaka kuingia kwenye nchi za Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef