Papa Francis ahiimiza Msumbiji kudumisha amani nchini humo
5 Septemba 2019Papa Francis ameanza siku yake ya kwanza ya ziara yake nchini Msumbiji leo kwa kupongeza mkataba wa amani kati ya serikali na kundi lililokuwa la waasi na kuonyesha mshikamano wake na wahanga wa vimbunga viwili vilivyotokea nchini humo.
Ziara yake nchini humo inajiri baada ya serikali na lililokuwa kundi la waasi la Renamo ambalo sasa ni chama kikuu cha upinzani kutia saini mkataba wa kihistoria. Pia inajiri baada ya taifa hilo kukumbwa na vimbunga viwili vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 600 na kuathiri maelfu ya wengine. Papa ametoa pole zake na kuonyesha umoja wake na wale wote walioathirika kutokana na vimbunga hivyo Idai na Kenneth ambavyo athari zake zinaendelea kushuhudiwa katika familia nyingi. Ameongeza kuwa angetaka waathiriwa hao kufahamu ushirikiano wake katika mateso wanayopitia na kujitolea kwa jamii ya kikatoliki kushughulikia hali hii ngumu zaidi .
Papa aliendelea kusema kuwa tayari amani imewezesha kuimarika kwa elimu na afya bora nchini Msumbiji na kuongeza kuwa kwa kuhakikisha amani inadumu kwa muda mrefu, ni muhimu kuangazia ujenzi wa makazi, ajira na kilimo. Msumbiji inatarajiwa kuandaa uchaguzi tarehe 15 mwezi Oktoba huku hali ikiwa ni ya hofu na kuongezeka kwa wasi wasi kuhusu kurejea kwa ghasia.
Rais Filipe Nyusi amesema kuwa juhudi zilizofanywa na raia wa Msumbiji pamoja na Papa Francis ni muhimu katika kulenga ujenzi wa taifa ambalo amani inakuwa jambo la kawaida ambapo siasa zinatekelezwa kupitia mashauriano na sio kwa kutumia bunduki. Rais Nyusi alimshukuru Papa Francis kwa usaidizi mkubwa aliotoa baada ya mikasa hiyo miwili ambayo taifa hilo inajaribu kujikwamua kutokana na athari zake.