Pence aonya wapiga kura wa Marekani
27 Agosti 2020Pence ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu katika mkutano uliokuwa na wafuasi wa Trump waliotaka kumuonyesha rais huyo kama bingwa wa maadili ya Marekani na haki za binadamu.
Wazungumzaji katika mkutano huo pia walizungumzia kuhusiana na nguvu za giza zinazolenga kuifikisha mwisho ndoto ya Marekani na wakasisitiza kwamba hawatopoteza uchaguzi huo kwa Warepublican.
Pence yeye alitoa hotuba yake kwa mkutano huo wa siku nne kutoka Baltimore katika eneo ambalo lilishuhudia Waingereza kuwashambulia kwa mabomu Wamarekani waliokuwa wanataka mabadiliko.
"Ukweli ni kwamba hamtokuwa salama katika utawala Joe Biden,” alisema Pence.
Akizungumzia rekodi nzuri za kiuchumi aliyokuwa nayo Trump kabla janga la virusi vya corona na juhudi zake zinazoendelea za kuufufua uchumi, Pence amewataka wapiga kura wajiulize, "ni nani munayemuamini kuufufua uchumi wenu? Mwanasiasa ambaye alikuwa uongozini wakati uchumi ulipofufuka kwa kasi ndogo kuwahi kushuhudiwa au kiongozi aliyeutengeneza uchumi mkubwa zaidi duniani?”
Hotuba ya Pence inakuja wakati ambapo kunashuhudiwa mwamko mpya wa mivutano ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani kufuatia kupigwa risasi kwa mtu mweusi Jacob Blake huko Kenosha Wisconsin.
Trump ametangaza kwamba anatuma vikosi zaidi kusaidia kutuliza machafuko katika mji huo baada ya watu wawili kuuwawa katika maandamano. Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 17 amekamatwa kwa mashtaka ya mauaji kutokana na vifo hivyo viwili.
Akizungumzia machafuko yanayoendelea sasa Pence amesema, "wacha niwe muwazi, machafuko ni lazima yaishe, iwe ni Minneapolis, Portland au Kenosha. Kutakuwa na amani na utiifu wa sheria katika kila sehemu ya nchi hii kwa kila mtu pasipo kujaribu rangi au tabaka,” alisema Pence.
Trump kupewa miaka mingine minne?
Pence amechukua jukumu la kutaka kuleta amani kwa njia ya utulivu kinyume na Trump ambaye ameonyesha kuwa anataka vitimbi kila wakati.
Wakati ugombea wa Trump 2016 ulipokumbwa na kashfa ya rekodi moja iliyoibuka ambapo rais huyo alisikika akijinaki kwa kuwadhalilisha wanawake kingono, ni Pence ndiye aliyemsaidia kutuliza mihemko ya Wamarekani iliyotokana na rekodi hiyo.
Makamu huyo wa rais anafanya jukumu muhimu sana kwa kuchaguliwa upya kwa Trump kwani anazunguka katika majimbo na miji muhimu kama Wisconsin kumpigia debe Trump.
Pence pia ameonyesha kuwa mtu wa pekee katika ikulu ya White House mwenye utulivu katika kipindi cha janga la virusi vya corona ambalo limewauwa zaidi ya Wamarekani 180,000 tangu makosa aliyoyafanya Trump mwanzoni kwa kusema kuwa virusi hivyo vitapotea tu.
Kura za maoni zinaonzesha kwamba karibu thuluthi mbili ya Wamarekani hawafurahii jinsi Trump alivyolishughulikia janga la virusi vya corona.
Kwa upande mwengine, mpinzani wa Pence, Kamala Harris wa chama cha Democratic atakuwa anamshambulia Trump kuhusiana na ushughulikiaji wake mbaya wa virusi vya corona siku ya Alhamis mjini Washington. Wakati huo huo Trump atakuwa anatoa hotuba yake ya kukubali uteuzi wa kugombea urais kutoka chama chake cha Republican.
Mwandishi: Jacob Safari
Mhariri: Josephat Charo