Wenye uchu waandamwe
20 Januari 2015Tuanzie lakini na ripoti ya shirika la misaada ya kiutu Oxfam kuhusu mwanya unaozidi kuwa mpana kati ya matajiri na masikini ulimwenguni.Gazeti la "Eisenacher Presse" linatahadharisha na kuandika:"Mwanya unaozidi kupanuka kati ya masikini na matajiri waliokithiri katika dunia hii ni kitisho.Kwanza unaleta ukosefu wa usawa katika jamii na pili unasababisha hatari kubwa kupita kiasi. Na hali hii haihusu pekee umaskini katika nchi za ulimwengu wa tatu bali pia unyonyaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya watu kutoka kile kinachotajikana kuwa nchi za magharibi.Sababu bila ya shaka ni ukosefu wa nidhamu.Hali hii ndio sababu ya kuchipuka wafuasi wa kila aina wa itikadi kali."
Wenye uchu wa kujitajirisha waandamwe
Gazeti la "Der neue Tag" linasema kuzifunga "pepo" za wanaokwepa kulipa kodi sio dawa.Gazeti linaendelea kuandika:""Kufungwa maeneo yanayowavutia wanaokwepa kulipa kodi za mapato,haimaanishi moja kwa moja kwamba utajiri wa dunia utagawanywa kwa njia za haki.Kwasababu anaetaka kupambana na umaskini anabidi kwanza awaandame wale wenye uchu wa kujitajirisha."
Uhuru wa vyombo vya habari
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na uhuru wa vyombo vya habari.Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linaandika:"Imedhihirika kutokana na kitisho kikubwa kinachozikumba haki za raia katika nchi za magharibi,kwa jinsi gani uhuru wa mtu kutoa maoni yake una thamani-na hali hii hailihusu jarida la Charlie Hebdo.Jarida ambalo kabla ya shambulio, halikuwa kitovu cha uhuru wa maoni nchini Ufaransa, badala yake lilikurubia kufilisika na kila kukicha likipoteza wanunuzi kutokana na msimamo wake mkali.Hali sawa na hiyo ya uhuru wa mtu kutoa maoni yake inawahusu wanaharakati wa Pegida na madai yao yasiyoeleweka.Kwamba kitisho cha mashambulio ya kigaidi kimewagutua hata wafuasi wanaopinga dini ya kiislam,hilo limedhihirika kutokana na uamuzi wao wa mara moja kutaka kuzungumza na vyama vya kisiasa,isipokua kile cha AfD.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga