1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIraq

Pentagon yaahidi kuendelea kuisaidia Iraq kupambana na IS

7 Machi 2023

Marekani imesema wanajeshi wake wako tayari kusalia nchini Iraq iwapo itakuwa tayari kushirikiana nao katika majukumu yasiyo ya kivita kwenye mapambano yake dhidi ya kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

https://p.dw.com/p/4OM5V
NATO Treffen Brüssel Lloyd Austin
Picha: AP

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema hayo akiwa ziarani nchini Iraq hii leo kuelekea maadhimisho ya miaka 20 tangu Marekani ilipoivamia Iraq na kuuangusha utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Saddam Hussein. 

"Wanajeshi wa Marekani wako tayari kubaki Iraq wakikaribishwa na serikali ya Iraq. Vikosi hivi vitashauri, vinasaidia na kuwezesha jukumu la kuunga mkono mapambano dhidi ya ugaidi yanayoongozwa na Iraq. Hii ni dhamira muhimu. Na tunajivunia kuunga mkono washirika wetu wa Iraq. Lakini lazima tuweze kushiriki kwa usalama ili kuiendeleza kazi hii muhimu," amesema Austin.

Austin ametoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari baada ya mkutano wake na waziri mkuu wa Iraq Mohammed al-Sudani mjini Baghdad. Ziara hii ya kushtukiza ya Lloyd inafanyika ikiwa ni miaka 20 tangu muungano wa kijeshi ukioongozwa na Marekani ulipouangusha utawala wa Saddam Hussein, baada ya kulivamia taifa hilo kufuatia madai ya aliyekuwa rais George Bush kwamba Iraq ina hifadhi kubwa ya silaha za maangamizi. 

Hatua hiyo ya kijeshi ya mwaka 2003 ilisababisha vifo vya maelfu ya raia wa Iraq na kusababisha ghasia ambazo kwa namna moja ama nyingine zilichangia kuibuka kwa kundi hilo linalojiita Dola la Kiislamu baada ya Marekani kuondoa wanajeshi wake mwaka 2011. Hata hivyo mwaka 2014, aliyekuwa rais Barack Obama alirejesha wanajeshi kuendeleza vita dhidi ya kundi hilo. Austin, ambaye ni afisa wa ngazi za juu zaidi katika serikali ya rais Joe Biden kuzuru Iraq, mwaka 2011 alikuwa mkuu wa vikosi vyote vya Marekani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Irak | Besuch US Verteidigungsminister Lloyd Austin
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin (kushoto) akifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani (kulia) wakati wa ziara yake nchini humo.Picha: Iraqi Prime Minister Media Office/REUTERS

Waziri mkuu Sudani kwa upande wake alisema kwenye taarifa kwamba mbinu inayochukuliwa na serikali yake inalenga kudumisha uwiano katika suala zima lia ushirikiano wa kikanda na serikali za kimataifa kwa kuzingatia maslahi ya pamoja na kuheshimu uhuru na kwa maana hiyo utulivu wa Iraq ni suala la msingi zaidi kuelekea usalama wa ukanda mzima.

Marekani kwa sasa ina wanajeshi 2,500 nchini Iraq na wengine 900 nchini Syria wanaosaidia kwa kuyashauri majeshi ya mataifa hayo yanaopambana na kundi hilo la IS, ambalo mwaka 2014 liliyadhibiti maeneo makubwa kwenye mataifa hayo.

Lakini kwa upande mwingine ziara ya Austin inalenga kumsaidia Sudani kukabiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa Iran nchini Iraq, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa zamani wa Iraq na baadhi ya wafuatiliaji wa mambo.

Soma Zaidi: Machafuko mapya yaikumba Iraq, Iran yafunga mpaka

Wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq mara kwa mara wamekuwa wakiwashambulia kwa maroketi wanajeshi wa Marekani na ubalozi wake mjini Baghdad. Mwaka 2020, Marekani na Iran al manusura ziingie kwenye mzozo kamili baada ya Marekani kumuua kamanda mkuu wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran Qassem Soleimani katika shambulio la ndege isiyotumia rubani.

Austin pia alitarajiwa kukutana na rais Nechirvan Barzani anayetawala mkoa wa Kurdistan nchini humo, katikati ya mzozo wa muda mrefu kati ya serikali ya kitaifa na ile ya kurdistan juu ya namna ya kushirikishana kwenye masuala ya bajeti na mapato yatokanayo na mafuta.

Tizama zaidi: