1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Peter Mutharika: Kutoka mshtakiwa wa uhaini hadi rais

31 Mei 2014

Peter Mutharika, ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Malawi siku ya Ijumaa, anajiandaa kuchukuwa hatamu ya uongozi wa taifa hilo maskini la kusini mwa Afrika chini ya kivuli cha mashtaka ya uhaini.

https://p.dw.com/p/1C9lG
Mshindi wa kinyanganyiro cha urais wa Malawi Peter Mutharika (katikati) akisalimiana na wafuasi wake.
Mshindi wa kinyanganyiro cha urais wa Malawi Peter Mutharika (katikati) akisalimiana na wafuasi wake.Picha: Gianluigi Guercia/AFP/Getty Images

Mutharika mwenye umri wa miaka 74 na nduguye rais wa zamani Bingu wa Mutharika alishinda kwa asilimia 36.4 ya kura dhidi ya asilimia 20.2 ya rais wa wasa Joyce Banda. Matokeo hayo yalitangazwa dakika chache baada ya mahakama ya juu kutupilia mbali jaribio la dakika za mwisho kuzuwia kutolewa kwake, ili kuruhusu kura zihesabiwe upya.

Mkuu wa tume ya uchaguzi Maxon Mbendera alimtangaza Mutharika kuwa "rais mteule" baada ya uchaguzi huo uliyofanyika wiki iliyopita, ambao rais Banda alidai ulikumbwa na kasoro nyingi na kuutangaza kuwa batili. Matokeo hayo yalionyesha kuwa Banda alitupwa katika nafasi ya tatu, akishindwa pia na Lazurus Chakwera wa chama cha Malawi Congress MCP, aliejipatia asilimia 27.8 ya kura.

Rais wa sasa Joyce Banda alipopiga kura yake.
Rais wa sasa Joyce Banda alipopiga kura yake.Picha: Reuters

Katika kivuli cha mashtaka ya uhaini

Mutharika sasa anajiandaa kuchukua hatamu ya uongozi chini ya kivuli cha mashtaka ya uhaini. Anatuhumiwa kujaribu kuficha kifo cha kaka yake akiwa ofisini miaka miwili iliyopita kwa lengo la kumzuwia Banda - ambaye wakati huo akiwa makamu wa rais, kuchukuwa madaraka.

Banda aliibuka kidedea na kuapishwa kuwa rais kama katiba inavyoagiza, akimuondoa serikalini waziri huyo wa zamani wa mambo ya kigeni, lakini Mutharika alimchachafya vibaya katika uchaguzi wa Mei 20.

Kiongozi huyo wa chama cha DPP Mutharika na maafisa wengine waandamizi wanakabiliwa na mashtaka mengine ya kuchochea uasi na kula njama za kufanya mauaji. Kesi hiyo bado haijaanza kusikilizwa, lakini wachambuzi wanasema kuna uwezekano mkubwa kwa kesi hiyo kuwekwa kando kwa sababu marais wa Malawi wanakuwa na kinga muda wote wanapokuwa madakarani.

Kibao cha "Cashgate" kumgeukia Banda?

Kuna fununu kuwa Mutharika atakapokuwa ofisini, anaweza akamgeuzia kibao Banda na kumshtaki kwa rushwa, kuhusiana na kashfa ya wizi wa dola za Marekani milioni 30 uliopewa jina la "Cashgate." Banda amedai sifa kwa kufichua kashfa hiyo, ambayo ilishuhudia fedha za msaada zikifujwa na wajanja serikalini. Lakini wakosoaji akiwemo Mutharika, wanasema fedha hizo zilienda kwenye kampeni ya chama chake.

Rais wa Zamani Hayati Bingu wa Mutharika.
Rais wa Zamani Hayati Bingu wa Mutharika.Picha: Reuters

Mutharika, profesa wa sheria ambaye aliishi kwa sehemu kubwa nje ya nchi, aliingia katika medani ya siasa ya Malawi mwaka 2009 alipochaguliwa kuwa mbunge na kuteuliwa waziri wa sheria. Baadaye alishikilia nyadhifa mbalimbali zikiwemo za elimu na masuala ya kigeni.

Amesema kuwa hatozingatia sera za uchumi wa kutoka juu kwenda chini, bali atakumbatia sera za uchumi wa kuanzia chini kwenda juu, zinazonuwia kuwaondoa watu kwenye umaskini na kuwaletea mafanikio. Msomi huyo aliegeuka kuwa mwanasiasa ana kibarua kigumu cha kujenga upya uchumi dhaifu wa taifa hilo, na kuwavutia wafadhili wa kigeni waliositisha sehemu ya msaada wao kufuatia sakata la "Cashgate."

Kitendawili cha uongozi wake

Mfumo wa uongozi wake serikalini, nje ya kivuli cha kaka yake mkubwa, bado ni kitendawili, wanasema wachambuzi. " Ni mtu mwenye maneno machache --- kwake hatuwezi kujua nini cha kutarajia," alisema Boniface Dulani kutoka chuo kikuu cha Malawi. "Hakuwa na ushawishi mkubwa wakati alipokuwa bungeni. Alikuwa akiongea kwa nadra."

Wakati Mutharika akiwa waziri wa elimu Chuo Kikuu cha Malawi kilikabiliwa na mgogoro, na kusababisha kufungwa kwa muda mrefu, baada ya wahadhiri watatu kufutwa kazi kufuatia matamshi waliyoyatoa darasani.

Ramani inayoonyesha mipaka ya kimataifa ya Malawi na mji mkuu wake Lilongwe.
Ramani inayoonyesha mipaka ya kimataifa ya Malawi na mji mkuu wake Lilongwe.Picha: DW

Mmoja alisema kuwa "Machipuko ya mataifa ya kiarabu" huenda yakaikumba Malawi. "Wakati wa kipindi hicho tete kilichohatarisha uhuru wa taaluma, Mutharika alishindwa kuonyesha uongozi," alisema Dulani. Baadaye alihamishiwa kwenye wizara ya mambo ya kigeni.

Peter Mutharika ni nani hasa?

Akiwa na shahada za sheria kutoka vyuo vikuu vya London na Yale, Mutharika aliondoka nchini Malawi katika miaka ya 1960 na kuweka makazi nchini Marekani. Alirejea nchini Malawi mwaka 1993 kusaidia kuandaa katiba ya kwanza ya kidemokrasia baada ya kuanguka kwa utawala wa dikteta Kamuzu Banda. Alirudi nchini Marekani lakini akarudi tena nyumbani mwaka 2004 baada ya kaka yake kuingia madarakani.

Akiwa mjane kwa miaka 30, Mutharika ana watoto watatu ambao wote wanaishi nchini Marekani. Kuchaguliwa kwake kunamfanya kuwa rais wa tano wa Malawi tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1964.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Caro Robi