PLO yasitisha ushirikiano wa usalama na Israel
6 Machi 2015Baraza Kuu la Chama cha Ukombozi wa Palestina – PLO limesema limefikia uamuzi huo kwa sababu Israel imekiuka makubaliano ya pande mbili, ikiwa ni pamoja na kuzuia mapato ya kodi inayokusanya kwa niaba ya Wapalestina.
Ahmad Abdelrahman, mwanachama wa PLO amesema. "Ushirikiano wote wa usalama kati ya mamlaka ya Palestina na Israel utasitishwa kwa sababu Israel imekiuka makubaliano yaliyosainiwa na pande zote mbili. Israel inapaswa kuyabeba majukumu yake yote kwa ajili ya watu wa Palestina katika ardhi inayokaliwa ya Palestina kwa mujibu wa sheria za kimataifa"
Msemaji wa Rais Mahmoud Abbas, ambaye analazimika kuchukua uamuzi rasmi wa kusitisha mahusiano ya usalama na Israel, hajazungumzia suala hilo na haifahamiki kama azimio hilo la Baraza Kuu la Palestina litaanza kutekelezwa au la.
Rais Abbas alilihutubia baraza hilo katika kikao cha ufunguzi siku ya Jumatano na akasema linapaswa kutathmini upya mahusiano yake na Israel baada ya kukwama mazungumzo ambayo yangemaliza mzozo wa Israel kuikalia ardhi ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki na Ukanda wa Gaza na kuruhusu uundwaji wa taifa la Palestina katika ardhi hiyo.
Afisa mmoja wa usalama wa Israel, aliyeulizwa kuhusu uamuzi huo, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa hakuna mabadiliko yoyote katika ushirikiano wa usalama.
Israel iisema mwezi Januari kuwa inazuia dola milioni 127 za mapato ya kila mwezi ya Palestina kama hatua ya kulalamikia uamuzi wa Abbas kuomba uwanachama katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na kuanzisha harakati za kuifungulia Israel mashtaka ya uhalifu wa kivita.
Fedha za kodi zinajumuisha karibu theluthi mbili ya bajeti ya Palestina na zinatumika kulipa maelfu ya wanafanyakazi wa sekta ya umma.
Kukamilika kwa makubaliano ya ushirikiano wa usalama, ambayo yalipatikana kupitia mikataba ya amani ya Oslo katikati ya miaka ya tisini, huenda kukawa na athari ya moja kwa moja kwa udhabiti wa miji ya Ukingo wa Magharibi kama vile Hebron, Nablus na Jenin ambako hutokea machafuko ya mara kwa mara ya kuipinga Israel. Majeshi ya Palestina pia huhitaji ruhusa ya Israel ili kuweka doria katika baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi ili kudumisha amani.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba