Poland, Slovakia na Hungary kuendeleza vizuizi vya nafaka
16 Septemba 2023Poland, Slovakia na Hungary zimetangaza kuwa zitaendea kuweka vizuizi vyao wenyewe katika uagizaji wa nafaka kutoka Ukraine. Uamuzi wa serikali za nchi hizo tatu umefikiwa, baada ya Tume ya Umoja wa Ulaya kutangaza kwamba haitopanua marufuku inayoathiri nchi tano za Umoja wa Ulaya ambazo ni jirani na Ukraine.
Marufuku hiyo iliyokuwa imetangazwa na Umoja wa Ulaya mwezi Mei iliziruhusu Poland, Bulgaria, Hungary, Romania na Slovakia kuzuia mauzo ya ndani ya ngano, mahindi na mbegu za alizeti kutoka Ukraine. Lakini nchi hizo ziliruhusu usafirishaji wa bidhaa hizo kuuzwa nje ya nchi zao.
Kamishna wa Biashara ndani ya Umoja wa Ulaya Valdis Dombrovskis alizitaka nchi hizo kujiepusha na hatua za upande mmoja dhidi ya marufuku ya uagizaji wa nafaka za Ukraine.