1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yakosolewa kuwarejesha wakimbizi kinyume cha sheria

30 Septemba 2021

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limesema kuwa Poland iliwarejesha kinyume cha sheria wahamiaji waliokuwa wamekwama kwenye mpaka wake na Belarus.

https://p.dw.com/p/413v6
Polen I Afghanische Flüchtlinge an der polnisch-weißrussischen Grenze gestrandet
Picha: Irina Polina/TASS/picture alliance

Taarifa hiyo imechapishwa leo kupitia uchunguzi uliofanywa wa picha za satelaiti na picha nyingine pamoja na video za Amnesty International. Shirika hilo limesema kwa kutumia picha za satelaiti za kuanzia Agosti 18, lilifanikiwa kugundua kurejeshwa kwa wahamiaji hao kutoka Afghanistan waliokuwa wamekwama kwenye mpaka huo kwa wiki kadhaa.

Eve Geddie, mkurugenzi wa Amnesty International barani Ulaya, amesema kitendo cha wahamiaji hao waliokuwa wakijaribu kuomba hifadhi kulazimishwa kuondoka bila kupatiwa mahitaji muhimu ni kinyume cha sheria za Ulaya na kimataifa.

Wahamiaji hawana maji wala chakula

''Amnesty International imekuwa ikifuatilia hali ya wahamiaji 32 waliokuwa wanatafuta hifadhi waliokwamba kwenye mpaka wa Poland na Belarus kwa wiki kadhaa bila ya kuwa na uwezo wa kupata chakula, maji safi, makaazi au dawa. Tumegundua kundi hili wakati mmoja lilikuwepo ndani ya ardhi ya Poland, ambako walirudishwa kwenda Belarus mwishoni mwa Agosti na walinzi wa mpakani wa Poland,'' alifafanua Geddie.

Geddie amesema Poland ina jukumu la kuwatathmini watu hao na kuona mahitaji yao yalikuwa yapi na iwapo walikuwa wanahitaji kupewa hadhi ya ukimbizi nchini humo. Amebainisha kuwa katika kundi la wahamiaji hao alikuwepo mtoto mwenye umri wa miaka 15. Amnesty International imesema wakimbizi hao walikimbia Afghanistan baada ya Taliban kuchukua madaraka.

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yameikosoa serikali ya Poland kutokana na jinsi inavyowahudumia wahamiaji walioko mpakani na kushindwa kuwapa msaada wa matibabu pamoja na chakula na malazi.

Migration I Belarus und Litauen
Wahamiaji wakiwa kwenye kambi ya Rudninkai, LithuaniaPicha: Mindaugas Kulbis/AP/picture alliance

Mwanzoni mwa mwezi huu, wahamiaji watatu walikufa wakiwa upande wa Poland wa mpaka na mmoja akiwa ndani ya mpaka wakati wakijaribu kuvuka kuingia Poland. Aidha, kifo cha tano cha mwanaume mmoja kutoka Iraq kiliripotiwa ndani ya Poland, kutokana na mshtuko wa moyo.

Amnesty International imetoa taarifa hiyo kabla ya mkutano wa Kamishna wa masuala ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Ylva Johansson na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Poland, Mariusz Kaminski mjini Warsaw kujadiliana kuhusu hali iliyoko kwenye mpaka wa Poland na Belarus.

Umoja wa Ulaya umependekeza kuweka vikwazo vikali zaidi vya visa kwa maafisa wa serikali ya Rais Alexander Lukashenko kutokana na kuongezeka tuhuma kwamba Belarus inawatumia wahamiaji kudhoofisha utulivu kwenye umoja huo wenye nchi 27.

Umoja wa Ulaya waguswa na hali za wakimbizi 

Wiki iliyopita Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilielezea wasiwasi wake kuhusu madhila wanayopitia wahamiaji waliokwama kwenye mpaka kati ya Poland na Belarus na iliitaka Poland kuyalinda maisha ya binadamu na kuliruhusu shirika la umoja huo la kulinda mipaka, Frontex kutoa msaada kwenye eneo hilo.

Poland imeufunga mpaka wake wenye urefu wa kilomita 418 na imetangaza hali ya hatari, huku maafisa wakiwapiga marufuku waandishi habari na mashirika ya kutoa misaada kuingia.

Wakati huo huo, Lithuania na Latvia zimeanza kujenga ukuta kwenye mpaka wake na Belarus ili kuzuia wahamiaji haramu kuingia. Lithuania inajenga ukuta wenye urefu wa kilomita 508, huku Latvia ikijenga wenye urefu wa zaidi ya kilomita 37. Poland, Lithuania na Latvia zimeripoti kuongezeka kwa kasi wahamiaji kutoka nchi kama vile Afghanistan na Iraq, wanaojaribu kuingia kwenye nchi hizo kupitia mipaka ya Belarus.

(DPA, AP, Reuters, DW https://bit.ly/2WtvAh0)