Polisi Kenya watawanya maandamno dhidi ya mswada wa fedha
6 Juni 2023Polisi ya Kenya ilifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wakiandamana karibu na majengo ya bunge kupinga mswada unaopendekezwa wa fedha. Kama utapitishwa kuwa sheria, mswada huo utaongeza ushuru kwenye bidhaa za mafuta na nyumba. Rais William Ruto, ambaye alishinda uchaguzi wa Agosti kufuatia ahadi ya kuwasaidia maskini, yuko chini ya shinikizo kuongeza mapato katika wakati ambao kuna ongezeko la ulipaji wa madeni ya serikali. Lakini mapendekezo yake yamekosolewa vikali na watumishi wa umma na wanasiasa wa upinzani, ambao wanasema gharama ya maisha tayari iko juu. Polisi iliwatawanya waandamanaji waliofika bungeni kuwasilisha waraka wa malalamiko kupinga mswada huo. Ruto anautetea mswada huo, akisema una vifungu vyake vinahitajika ili kuhakikisha utulivu wa kifedha na kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana kupitia ujenzi wa nyumba mpya utakaofadhiliwa na ushuru wa nyumba.