Polisi wamkamata baba kwa madai ya kumuua bintiye
4 Agosti 2020Waswahili husema ukicha mwana kulia utalia wewe, huku jamii ya Kiafrika ikichukulia kiboko kama mbinu mojawapo ya kumrekebisha mtoto kimaadaili.
Hata hivyo, ni kiwango kipi kitatajwa kama kupitilizwa kwa adhabu endapo mzazi atamuadhibu mtoto wake?
Tukio la baba mzazi mwenye umri wa miaka 48 Maurice Owaga Owino kumuadhibu mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 15, kichapo kinachodaiwa kusababisha kifo cha mtoto huyo na kumuacha mwenzake wa miaka 14 na majeraha ya kupitiliza ni tukio ambalo limeibua kauli nyingi miongoni mwa raia katika eneo hili, wengi wakiwemo wazazi na wataalamu wa maswala ya kiakili wakitoa maoni mbali mbali.
Katika tukio hilo, Owino anadaiwa kuwapa kichapo watoto wake wawili wa kike baada ya kuondoka nyumbani asubuhi ya siku ya Ijumaa wiki iliyopita bila kuomba ruhusa ya baba yao na ni hapo waliporudi nyumbani kwao kijijini Geyo, eneo bunge la Muhoroni jimboni Kisumu majira ya jioni wakakumbana na kichapo hicho anavyosimulia mama ya watoto hao, Benter Owino.
Katika juhudi za kuficha ukweli halisi wa chanzo cha kifo cha mtoto wake, jamaa katika boma la mzee huyo wameeleza kuwa, baba huyo alinunua jeneza siku ya Jumamosi lakini juhudi za kuuzika mwili ziligonga mwamba baada ya naibu chifu kijijini humo kukataa kutoa cheti cha mazishi bila barua ya daktari na hapo akaibua yaliyotokea.
Afisa msimamizi wa afya ya kiakili hospitali kuu ya jimbo la Kisumu Faith Juma anasema huenda msongo wa changamoto za kimaisha ukawa umehusika katika kuibua hasira za kupitiliza miongoni mwa watu na kuishia kutekeleza matukio ambayo baadae wataishia kujutia kauli sawia ikiungwa na baadhi ya wazazi niliosema nao.
Mshukiwa anatazamiwa kuwasilishwa mahakamani kujibu mashtaka ikizingatiwa kuwa, nchini Kenya kikatiba, adhabu ya kuwapiga watoto ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za watoto.