Mashirika ya haki za binadamu yalia na Polisi Kenya
16 Oktoba 2017Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Kimataifa,Human Rights Watch na Amnesty Internationa yametowa ripoti ya pamoja kuhusu kenya ikisema kwamba polisi nchini humo imeua kiasi watu 33 na pengine zaidi ya 50 na kuwajeruhiwa mamia ya wengine katika baadhi ya maaneo ya mji mkuu Nairobi ,katika hatua ya kuyakabili maandamano yaliyozuka kufuatia uchaguzi wa tarehe 8 Agosti mwaka huu.
Ripoti ya mashirika hayo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ina kurasa 37 ikibeba kichwa cha maneno kinachosema wauwe wale wahalifu:Vikosi vya usalama na ukiukaji katika uchaguzi wa Agosti nchini kenya. Ripoti hii inaeleza juu ya polisi walivyotumia nguvu nyingi na wakati mwingine sio polisi tu walikuwepo mawakala wa mashirika ya usalama ambao walipambana na waandamanaji na wakaazi katika maeneo ambayo ni ngome ya upinzani baada ya uchaguzi huo mjini Nairobi.
Polisi wamehusishwa moja kwa moja katika mauaji ya kiasi watu 33 kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika. Watu wengine 17 wamedaiwa kuuwawa wengi katika mtaa wa Kawangware ingawa waliofanya uchunguzi huu hawakuweza kuthibitisha kuhusu kilichotokea kuhusu kuuwawa watu hao 17. Michelle Kagari naibu mkurugenzi wa Amnetsy International kanda ya Afrika Mashariki, pembe ya Afrika na eneo la maziwa makuu anasema watu wengi waliuwawa na wengine zaidi wakaachwa na majeraha yaliyowatia ulemavu wa maisha katika mashambulio yaliyofanywa na polisi dhidi ya wafuasi wa upinzani.
Kuna binti wa miaka 9 Stephanie Moraa Nyaragi alipigwa risasi akiwa amesimama kibarazani katika nyumba yao ya ghorofa. Jeremiah Maraga mlinzi mwenye umri wa miaka 50 alipigwa na polisi hadi kuuwawa. Lilian Khavere akiwa na ujauzito wa miezi minane alikanyagwa hadi akafariki na watu waliokuwa wakikimbia fujo. Hayo ni baadhi ya matukio yaliyoorodheshwa kwenye ripoti hiyo.
Walioendesha uchunguzi waligundua kwamba licha ya polisi kuonesha kufanya kazi yao vyema wakati fulani katika maeneo mengi mengine walihusika moja kwa moja kuwapiga risasi au kuwateremshia vipigo hadi kuua waandamanaji. Wahanga wengine walifariki kutokana na kushindwa kupumua baada ya kuvuta gesi nyingi ya kutowa machozi na maji ya pilipili yaliyokuwa yakitumiwa na polisi.Makopo ya gesi ya kutowa machozi yalikuwa yakirushwa kwa karibu sana dhiudi ya waandamanaji.
Kuna pia waliopoteza uhai kufuatia kukanyagwa na makundi ya watu waliokuwa wakikimbia fujo.Wachunguzi wa Amnesty Internationa na Human Rights watch waliwahosji wahanga 151,mashahidi,wanaharakati,wafanyakazi wa mashirika ya msaada na polisi katika maeneo ya watu wa kipato cha chini jijini Nairobi ambako ndiko waliko wafuasi wengi wa upinzani.Kabla ya uchaguzi wa Agosti nane polisi walishayaweka alama maeneo haya kuwa ni maeneo tete ambako kuna uwezekano wa kutokea vurugu na walipeleka askari chungunzima na kuongeza hali ya wasiwsi.
Kabla ya Human Rights Watch kuanza uchunguzi tayari lilikuwa limeshaorodhesha matukio ya kuuliwa watu 12 na polisi kufuatia maandamani magharibi mwa Kenya.Tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Kenya ilitowa ripoti yake iliyoonesha kwamba watu 37 wameuwawa nchini humo,ambapo visa vya kuuwawa watu 33 vimeorodheshwa katika ripoti ya pamoja na Human Rights Watch na Amnesty International.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman
Source:HRW/Amnesty International