1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Kenya yawasambaratisha waandamanaji

8 Agosti 2024

Polisi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaomtaka rais ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/4jGE1
Makabiliano kati ya polisi ya Kenya na waandamanaji
Makabiliano kati ya polisi ya Kenya na waandamanaji.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Maandamano hayo ya Nairobi yaliandaliwa na wanaharakati waliokasirishwa na Rais William Ruto hata baada ya kuwatimua karibu mawaziri wake wote na kuwaongeza viongozi wa upinzani katika kile alichokiita serikali pana.

Maduka yalifungwa na magari ya usafiri wa umma yakajizuia kuingia katikati ya mji kama ilivyo kawaida.

Polisi pia waliweka vizuizi kwenye barabara za kuingia mjini. Miji mikubwa, ukiwemo wa Kisumu ambao ndio ngome ya upinzani ambayo katika siku nyuma ulishuhidia maandamano, ulisalia tulivu huku baadhi ya wakaazi wakiwaambia waandishi habari kuwa hawajaandamana kwa sababu vigogo wa upinzani wamejumuishwa serikalini.

Hayo yalijiri wakati Rais Ruto akishuhudia kuapishwa kwa baraza lake jipya la mawaziri katika Ikulu ya Nairobi.