Polisi ya Ujerumani yasema idadi ya wanaovuka mpaka yapungua
31 Oktoba 2024Polisi nchini Ujerumani imesema kuwa imegundua kupungua kwa asilimia 13 ya watu wanaovuka mpaka kinyume cha sheria katika kipindi cha wiki tatu za kwanza tangu kuanza kwa ukaguzi wa kudumu wa mipakani, ikilinganishwa na wiki tatu zilizopita kabla ya kuanza kwa zoezi hilo. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za polisi zilizotolewa leo Alhamisi,
Takwimu za Polisi wa Shirikisho zilizoonyeshwa kwa shirika la habari la Ujerumani la Dpa zimeainisha kuwa jumla ya wahamiaji 3,464 walijaribu kuingia bila ruhusa katika mipaka ya Ujerumani kati ya Septemba 16 na Oktoba 6.
Soma zaidi : Hakuna Imani!: Muungano tawala Ujerumani waendelea kuwa njiapanda
Kati ya hao, 2,073 walirudishwa kwenye mpaka. Katika kipindi cha kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 15 huku kukiwa na watu 3,984 walioingia, ambao hawakuidihinishwa na 2,353 walikataliwa.
Takwimu hizo zinajiri siku chache baada ya uchunguzi wa bunge kuwasilishwa na mbunge Clara Bünger wa chama cha siasa za mrengo wa kushoto cha Die Linke aliyemtaka waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani kusitisha zoezi hilo.
Polisi wa Shirikisho wamekuwa wakifanya ukaguzi katika mipaka ya Ujerumani inayopakana na Ufaransa, Luxembourg, Ubelgiji, Uholanzi na Denmark tangu Septemba 16.
Ukaguzi wa kushtukiza unaendelea
Ukaguzi wa kushtukiza umekuwa ukifanyika pia katika mipaka ya Ujerumani na Poland, Jamhuri ya Czech na Uswizi tangu katikati mwa mwezi Oktoba 2023, ingawa sio kila msafiri anachunguzwa katika msako huo.
Soma zaidi : Ujerumani na Umoja wa Ulaya zalaani kunyongwa Raia wa Ujerumani mwenye asili ya Iran
Tangu kuanzishwa kwa ukaguzi huo idadi ya watu wanaoingia bila idhini kwenye mipaka na Luxembourg, Ubelgiji na Uholanzi imeongezeka.
Katika mpaka wa Ujerumani na Ufaransa, ambapo huko tayari ukaguzi ulizidishwa mwaka huu kutokana na michuano ya mataifa ya Ulaya iliyofanyika hapa Ujerumani kiwango cha watu kuingia kiholela kimepungua kutoka 766 hadi 567:
Soma zaidi : India na Ujerumani zakubaliana kuzalisha nishati safi
Udhibiti wa mipaka kwa ujumla unaenda kinyume na masharti yaliyoainishwa na makubaliano ya Eneo la Schengen ambapo watu wenye visa ya Schengen wanaweza kusafiri katika nchi zote za Ulaya zilizopo kwenye eneo hilo.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser aliidhinisha ukaguzi katika mipaka yote ya Ujerumani huku Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ikiunga mkono mchakato huo ikisema kuwa ni muhimu kudhibiti uhamiaji usio wa msingi, uhalifu na kulinda amani dhidi ya ugaidi.
Polisi wanamtazama mtu anayejaribu kuvuka mpaka kama mhamiaji haramu ikiwa atajaribu kuingia Ujerumani bila kibali halali cha makaazi. Kwa mujibu wa serikali ya shirikisho, polisi wanaruhusiwa kumrudisha kama mtu huyo hajawasilisha maombi ya kuomba hifadhi na ikiwa kuna marufuku ya muda ya kuingia nchini Ujerumani kwa muda huo.