1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yamtia mbaroni kiongozi maarufu wa upinzani Tanzania

19 Septemba 2024

Wanaharakati, wachambuzi na wadau wa siasa, wametoa maoni yao kuhusu kamatakamata ya viongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania CHADEMA;

https://p.dw.com/p/4kpS0
Tansania Ex-Chadema-Bürgermeister Boniface Jacob von Polizei verhaftet
Meya wa zamani kutoka chama cha Chadema Tanzania Boniface Jacob.Picha: Florence Majani/DW

Wadau hao wanasema mwenendo huo unaweza kuchagiza kuvunjika kwa amani na kuiweka rehani demokrasia na utawala bora katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mtazamo huu wa wanaharakati na wadau wa siasa wameuelezea siku moja tu baada ya kada wa Chadema na Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniphace Jacob, maarufu Boni Yai, kukamatwa jana na jeshi la polisi.

Kutiwa mbaroni kwa kiongozi maarufu wa CHADEMA

Tansania Ali Mohamed Kibao Chadema
Mwanachama wa Chadema Ali Mohamed Kibao aliyeuwawa katika mazingira ya utatanishi nchini Tanzania.Picha: Chadema

Jacob, alikamatwa jioni ya 18.09.2024 akiwa katika mgahawa mmoja jijini hapa, na nyumba yake kupekuliwa kwa takribani dakika 180, kabla ya kupelekwa polisi, ambako dhamana yake iligonga mwamba, na hivyo akalala rumande.

Baadaye, Jeshi la Polisi, kupitia Msemaji wake, David Misime, walisema wanamshikilia Jacob kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya jinai.

Ukiachilia mbali kukamatwa kwa Jacob, juzi Septemba 16, Jeshi la polisi lilimwandikia wito wa kufika kituo cha Polisi Kinondoni, kwa ajili ya mahojiano, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Majibu ya polisi kuhusu kuhitajika kwa Mnyika

Katika taarifa ya polisi, ilyosainiwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum, SSP Davis Msangi,  Mnyika aliitwa polisi kwa ajili ya mahojiano yanayohusiana na uchunguzi kuhusu kifo cha Ali Kibao, kada wa Chadema, aliyetekwa na kisha kuuawa, mwanzoni mwa mwezi huu.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kintikwi, alipoulizwa kuhusu kiini hasa cha Mnyika kuitwa kwa mahojiano, alisema; "Siku akija, yeye umuulize kuwa aliitiwa nini”

Kamata kamata hii imeiwaibua wanaharakati na wapembuzi yakinifu hapa nchini ambao kwanza, wamelaani namna jeshi la polisi linavyokamata. Profesa Ibrahim Bakari, ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema "Kwa vile taswira ya polisi na vyombo vingine vya usalama imechafuka kwa hivyo wanakamata watu kuonesha kuwa ni wahalifu hata kama hakuna uhalifu huo.

Soma zaidi:Polisi ya nchini Tanzania imeyazuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa Septemba 23

Pamoja na hao, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC, nacho kimetoa tamko kikionyesha kushtushwa na matukio hayo ya kupotea na ukandamizaji unaoelekezwa kwa wanaharakati wa haki za binadamu wanaotumia mitandao ya kijamii.

Haya yanajiri wakati Tanzania ikijiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu na uchaguzi mkuu, Oktoba, 2025.

DW. Dar es Salaam