1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo akutana na waziri mkuu wa India

26 Juni 2019

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amekutana na waziri mkuu wa India Narendra Modi, katika juhudi za kulinda uhusiano kati ya mataifa hayo licha ya mzozo wa kibishara unaoendelea kati ya mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/3L6o6
USA Außenminister Pompeo reist nach Saudi-Arabien
Picha: picture-alliance/dpa/J. Martin

Kama taifa kubwa la kidemokrasia linalofunikwa na China ya kiimla, India ni mshirika muhimu wa Marekani katika juhudi zake za kukabiliana na kuibuka kwa China, na mwaka 2016, Marekani iliiorodhesha India kama mshirika muhimu katika suala zima la ulinzi.

Lakini sera ya Rais Donald Trump ya Amerika Kwanza na matumizi yake ya haraka ya ushururu - katika kile anachosema ni juhudi za kurejesha ajira nchini Marekani - vimeikasirisha serikali mjini New Delhi.

Pompeo na Modi hawakufanya mkutano na waandishi habari lakini waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alitarajiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari baadae Jumatano.

Wakosoaji wanasema uhusiano kati ya Marekani na India ni mgumu hasa kutokana na ukweli kwamba hata India yenyewe ina sera yake ya kulinda biashara za ndani, inayoelezwa mara nyingi kupitia ukiritimba unaozuwia kampuni za kigeni kushindana katika soko lake kubwa la zaidi ya watumiaji bilioni moja.

Mike Pompeo in Saudi Arabien
Waziri Pompeo alikuwa nchini Saudi Arabia alikokutana na mwanamfalme Muhammad bin Salman, Juni 24, 2019.Picha: Getty Images/J. Martin

Maandalizi ya mkutano kati ya Trump na Modi

Mazungumzo ya Pompeo na Modi mjini New Delhi maepma Jumatano yalikuja kuelekea mkutano wa waziri mkuu huyo wa India na rais Donald  Trump kwenye mkutano wa kilele wa mataifa yalioendelea na yanayoinukia kiuchumi ya G20, unaofanyika nchini Japan baadae wiki hii, ambao unatazamiwa kugubikwa na ushuru wa bidhaa za kigeni.

Mwaka uliopita Marekani ilikataa kuiondoa India kwenye mpango wa utozaji ushuru kwenye bidhaa za chuma na bati. Uhusiano ulidorora zaidi mwezi Juni baada ya Marekani kusitisha hadhi ya upendeleo wa kibiashara kwa India, ambayo iliiwezesha nchi hiyo kubwa ya Asia kuuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 6 zisizotozwa ushuru nchini Marekani kila mwaka.

India ilijibu kwa kutangaza ushuru wake yenyewe kwenye bidhaa 28 kutoka Marekani, zikiwemo malozi, matufaha na jozi - bidhaa ambazo ni muhimu sana kwa wapigakura waTrump katika maeneo ya vijijini.

Pompeo aliwasili India Jumanne akitokea nchini Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Afghanistan, katika ziara iliyolenga kujenga ushirikiano wa kimataifa kukabiliana na Iran.

Maafisa wa India wanasema wana tofauti kidogo na Marekani kuhusu masuala ya kisiasa na kimkakati likiwemo suala la Iran, lakini wametadharisha kwamba mataifa hayo mawili yanahitaji kuwa makini kuhusu biashara.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, ape

Mhariri: Zainab Aziz